Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Mkataba wa Huduma kwa Wateja “Client Service Charter” wa Tume ya Utumishi wa Umma, utawezesha wadau kufahamu huduma zitolewazo na Tume.

Mkataba wa Huduma kwa Wateja ni ahadi na mapatano baina ya Mtoaji na Mpokeaji wa huduma. Mkataba unabainisha viwango vya utoaji huduma ambavyo mpokeaji wa huduma atavitarajia. Kupitia Mkataba huu, Wateja na Wadau wa Tume watapata fursa ya kufahamu huduma zitolewazo na Tume.

Mkataba unaonesha namna Tume itakavyo wajibika moja kwa moja kwa wateja wake. Aidha, ni njia bora ya kuibua na kushughulikia malalamiko na taarifa nyingine za wateja kuhusu viwango vya huduma inayotolewa. Mkataba huu umeandaliwa kwa kuzingatia Mwongozo uliotolewa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wa namna ya kuandaa Mkataba wa huduma kwa Wateja katika Utumishi wa Umma na kwa kuzingatia maoni ya Wadau na Watumishi wa Tume.

Kupitia Mkataba huu, Tume itajipima mara kwa mara na kufuatilia utendaji wake ili kuboresha huduma zake kwa Umma. Tume ya Utumishi wa Umma inapenda kuwa mfano katika kuzingatia viwango vya huduma vilivyowekwa. Mrejesho kuhusu huduma tunazotoa utakuwa ni muhimu katika kuinua viwango vya utendaji na kuamsha ari ya kazi, uelewa, uwazi na uwajibikaji miongoni mwa watumishi wa Tume.

Tume ya Utumishi wa Umma inatambua umuhimu wa kutumia tamko la huduma kwa mteja ili kumlenga zaidi mteja katika utoaji wa huduma zake kwa Umma. Ni matumaini ya Tume kuwa mtatumia Mkataba huu kwa mawasiliano na Tume katika kutimiza lengo la kufanya tathmini na kuboresha utoaji wa huduma.

Tume, inaamini kuwa itapata ushirikiano wa Wateja na Wadau wake kwenye kutimiza azma ya Mkataba huu wa Huduma kwa Wateja katika kuleta mafanikio na kufikia malengo ambayo imejiwekea.

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.