Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Kutoa Miongozo katika masuala ya Rasilimali Watu

1.0 UTANGULIZI

Tume ya Utumishi wa Umma imeundwa chini ya Kifungu Na. 9(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na.18 ya mwaka 2007. Jukumu la msingi la Tume ni Kurekebu (regulate) Utumishi wa Umma nchini ili kuimarisha Utawala Bora na Uwajibikaji kwa Viongozi na Watumishi wa ngazi zote katika Utumishi wa Umma. Kwa sababu hiyo, kazi kubwa ya Tume ni kufuatilia na kusimamia Utumishi wa Umma ili kuhakikisha kuwa Utumishi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.

2.0 MAMLAKA YA TUME
Kifungu 10 (1) (C) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 18 ya mwaka 2007 kimeipa Tume ya Utumishi wa Umma uwezo wa kutoa Miongozo na kufuatilia Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Nyaraka katika Utumishi wa Umma.

3.0 MAANA YA MWONGOZO
·   Mwongozo ni maelekezo maalum au Ufafanuzi wa namna ya kutekeleza jambo fulani.
·   Ni njia ya kupitia ili kufikia mahali palipokusudiwa kwa ufanisi unaotakiwa.
·   Miongozo inayotolewa na Tume ni maelekezo maalum kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu, ili kutekeleza kwa ufanisi masuala yanayohusu Rasilimali Watu kulingana na kazi au Mamlaka zao.
·   Miongozo ya Tume ya Utumishi wa Umma iliyotolewa imesaidia sana Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kutekeleza wajibu wao kama inavyotakiwa kwa hiyo kuongeza viwango vya uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Nyaraka ziliyopo.
·   Aidha, Miongozo imesaidia Tume katika kufuatilia na kusimamia vizuri Utumishi wa Umma.

4.0 MADHUMUNI YA MWONGOZO
Madhumuni ya Mwongozo ni kuwepo kwa tafsiri na uelewa wa pamoja kuhusu utekelezaji wa ni Sheria, Kanuni, Taratibu na Nyaraka za masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma.

4.1. Faida ya Mwongozo
Zipo faida za kuwa na Mwongozo kwa Watendaji na Wasimamizi wa masuala ya Rasilimali Watu kwenye Utumishi wa Umma. Faida hizo ni kwamba Mwongozo:-

Una jambo moja mahsusi lililotolewa maelekezo (Specific).
Hutumia lugha nyepesi (simple).
Mpangilio ni rahisi (systematic).
Hutoa maelekezo yaliyo wazi (clear).
Hutoa ufafanuzi kuhusu jambo ambalo halikuwekwa bayana kwenye Sheria, Kanuni au Taratibu (clarity).
Rahisi kutumia na kueleweka (comprehensible).
Rahisi kubebeka (portable).
Haupotezi muda (timekeeping).
Kwa kuzingatia madhumuni na faida za Mwongozo, tunaona haja ya kuwa  na Miongozo.

5.0 MIONGOZO ILIYOTOLEWA NA TUME YA UTUMISHI WA UMMA
Tume ya Utumishi wa Umma imeweza kutoa Miongozo Mbalimbali kama ifuatavyo:

·   Mwongozo Kuhusu Masuala ya Ajira Katika Utumishi  wa Umma Toleo, Na.1 la mwaka 2004.
·   Mwongozo Kuhusu Masuala ya Ajira Katika Utumishi wa Umma Toleo, Na. 2 la mwaka 2009.
·   Mwongozo Kuhusu Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Watumishi wa Umma, Toleo Na.1 la mwaka 2005.
·   Mwongozo kuhusu Taarifa za Kuwasilisha Tume, Toleo Na. 1 la mwaka 2005.
·   Mwongozo Kuhusu Mashauri ya Nidhamu na Rufaa kwa Watumishi wa Umma, Toleo Na.2 la mwaka 2009.
·   Mwongozo Kuhusu Ukaguzi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma, Toleo Na. 1 la mwaka 2009.
·   Maelekezo Mahsusi Kwa Mamlaka za Nidhamu na Kamati za Uchunguzi kuhusu namna ya Kuendesha Uchunguzi wa Mashauri ya Nidhamu Na.1 ya mwaka  2008.

Tume huboresha au huuisha miongozo kutokana na mabadiliko mbalimbali ya
Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma zinazotolewa na Serikali,
changamoto za utekelezaji wa masuala ya kiutumishi, mawazo ya wadau na
haja ya kuweka bayana jambo fulani.

6.0 MAHITAJI NA HATUA MUHIMU KATIKA KUANDAA MWONGOZO

6.1 Mahitaji
Ili Mwongozo uandaliwe sharti kuwe na mambo yafuatayo:

Suala/ Jambo linalohitaji kutengenezewa Mwongozo (issue).
Nyenzo Muhimu.
Wahusika.

6.1.1 Suala au jambo linalohitaji kutengenezewa Mwongozo
Suala /Jambo hilo linaweza kusababishwa na:-

Tafsiri tofauti na utekelezaji unaotofautiana kuhusu jambo moja kati ya watekelezaji. (Mamlaka za Ajira, Nidhamu au Mwajiri n.k.).
Kukiukwa mara kwa mara kwa Sheria, Kanuni, Taratibu au Nyaraka.
Kukosekana kwa maelezo kuhusu utekelezaji wa jambo fulani (Gaps).

6.1.2   Nyenzo Muhimu
Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Nyaraka mbalimbali zinazohusu uendeshaji wa Utumishi wa Umma ni nyenzo muhimu zinazotumika katika kuandaa Mwongozo. Aidha, Mwongozo ni lazima uandaliwe kwa kuzingatia nyenzo hizo zinazohusu uendeshaji wa Utumishi wa Umma bila kukinzana au kwenda kinyume nazo.

6.1.3 Walengwa/Kundi linaloandaliwa Mwongozo

  • Mwongozo huandaliwa kwa kulenga kundi fulani. Kundi hilo  litakuwa limepewa mamlaka/ kazi ya kutekeleza jambo fulani hivyo, maelekezo huwaongoza kujua namna ya kutekeleza kwa ufanisi madaraka/kazi yao.
  • Kundi hilo linaweza kuwa baadhi ya watumishi wa Umma, Waajiri, Mamlaka za Ajira, Mamlaka za Nidhamu, Wakaguzi wa rasilimali watu au kundi lolote.

7.0 SIFA ZA MWONGOZO
Ili Mwongozo utambulike na kukubalika ni lazima utimize sifa za kuweza kuitwa Mwongozo. Sifa za Mwongozo ni pamoja na:

·   Kuwa na jina/jambo linalotolewa maelekezo.
·   Kuonesha Mamlaka iliyoutoa.
·   Kueleza nguvu ya kisheria ya chombo kilichotayarisha Mwongozo.
·   Kuwa na namba na mwaka wa kutolewa.
·   Kuwa na dibaji.
·   Kuainisha wahusika wa Mwongozo huo.
·   Kuwa na saini ya mwenye mamlaka.
·   Kutaja tarehe ya kuanza kutumika.
·   Kuwa na utangulizi.
·   Kueleza madhumuni ya Mwongozo huo.
·   Kutoa maelekezo kwa ufasaha.
·   Kuwa na viambatisho.

8.0 HITIMISHO
Vyombo vilivyopewa jukumu la kusimamia rasilimali watu vina wajibu wa kuona kuwa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazingatiwa kwa viwango vya hali ya juu katika kuendesha Utumishi wa Umma. Aidha, ni wajibu wa vyombo hivyo kuona umuhimu wa kuwasaidia watendaji kwa kutoa Miongozo ili kuhakikisha uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika kuimarisha Utawala Bora.

 

 

 

 

 

   

Taarifa Kwa Vyombo vya Habari

31-05-2022

TAARIFA KWA UMMA

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.