Ukaguzi wa Ndani
Ukaguzi wa Ndani
MAJUKUMU YA KITENGO CHA UKAGUZI WA NDANI KWA KULINGANA NA KANUNI YA 29 YA KANUNI ZA FEDHA ZA MWAKA 2001, BAADA YA KUREKEBISHWA MWAKA 2024.
(A) Majukumu ya Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani yapo kwa madhumuni ya kutathmini udhibiti uliopo katika matumizi ya rasilimali na shughuli za Taasisi -
- Kukagua na kutoa Taarifa juu ya udhibiti sahihi wa upokeaji, uhifadhi na matumizi ya rasilimali zote za Taasisi;
- Kupitia na kutoa taarifa juu ya usahihi wa taratibu za fedha na uendeshaji zilizowekwa katika sheria yoyote au kanuni yoyote au maagizo ya udhibiti wa mapato na matumizi ya Taasisi;
- Kupitia na kutoa taarifa juu ya uainishaji, ugawaji na matumizi sahihi ya hesabu za mapato na matumizi;
- Kukagua na kutoa taarifa kuhusu uaminifu na uadilifu wa data za fedha na zile zinazotumika katika majukumu mengine ya Taasisi kwenye kuandaa taarifa za fedha na ripoti nyinginezo;
- Kupitia na kutoa Taarifa juu ya mifumo iliyopo kwa ajili ya kulinda mali za Taasisi na, inapobidi, kuthibitisha kuwepo kwa mali hizo;
- Kukagua na kutoa ripoti kuhusu ukaguzi maalum kuhusu thamani ya fedha, utendaji kazi, usalama wa taarifa, ulinzi wa data na usalama wa mtandao na uchunguzi wa kimahakama;
- Kukagua na kutoa ripoti juu ya shughuli au programu ili kuhakikisha kama matokeo yanaendana na malengo yaliyowekwa;
- Kupitia na kutoa taarifa juu ya utoshelevu wa hatua za menejimenti kwa ripoti za ukaguzi wa ndani na nje na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo ya ukaguzi;
- Kukagua na kutoa Taarifa juu ya utoshelevu na ufanisi wa udhibiti ndani wa mifumo ya kompyuta ya taasisi;
- Kupitia na kutoa taarifa juu ya utekelezaji wa udhibiti wa vihatarishi kwa kila robo Mwaka na kila Mwaka;
- Kuwasilisha Taarifa za Ukaguzi wa Ndani za robo Mwaka kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ndani ya siku thelathini baada ya kumalizika kwa robo husika baada ya kuhakikiwa na Kamati ya Ukaguzi na kuidhinishwa na Afisa Masuuli;
- Kuwasilisha ripoti za Mwaka za Ukaguzi wa Ndani kwa Mkaguzi Wa Ndani Mkuu wa Serikali ndani ya siku thelathini baada ya mwisho wa Mwaka wa fedha, hii ni baada ya kuhakikiwa na Kamati ya Ukaguzi na kuidhinishwa na afisa masuuli, na
- Kuwasilisha Mpangokazi unaozingatia vihatarishi kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali ndani ya siku thelathini kabla ya kuanza kwa Mwaka wa fedha, baada ya kuhakikiwa na Kamati ya Ukaguzi na kuidhinishwa na Afisa Masuuli.
B) Kazi za Kitengo cha ukaguzi wa Ndani zitahusisha;
- Kukagua utekelezaji wa masuala ya udhibiti wa vihatarishi mara kwa mara kama ilivyoainishwa katika Mwongozo wa usimamizi wa vihatarishi wa taasisi ya umma;
- Kwa madhumuni ya kanuni ndogo ya (1)(j), (k) au (l), Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kitawasilisha Taarifa kwa Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali pale Afisa Masuuli au Kamati ya Ukaguzi haijapitia au kuidhinisha Taarifa ya Ukaguzi wa Ndani au Mpangokazi ndani ya siku thelathini baada ya mwisho wa robo husika au ndani ya siku thelathini kabla ya kuanza kwa mwaka wa Fedha, kama itakavyokuwa.
C) Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani kitatathmini na kutoa mapendekezo yanayofaa ili kuboresha taratibu za usimamizi wa Taasisi kwa-
- Kufanya maamuzi ya kimkakati na ya kiutendaji;
- Kukuza maadili yanayofaa ndani ya taasisi, na
- Kuhakikisha usimamizi bora wa utendaji na uwajibikaji;