Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Historia ya Tume ya Utumishi wa Umma

HISTORIA YA TUME YA UTUMISHI WA UMMA

 

UTANGULIZI

Kihistoria, Tume ya Utumishi wa Umma ni matokeo ya maboresho mbalimbali yaliyoanzishwa na Serikali kwa lengo la kuufanya Utumishi wa Umma uongeze ufanisi, uwajibikaji na tija katika utoaji huduma kwa wananchi kwenye miaka ya 1990 na kabla yake. Maboresho hayo kwa nyakati tofauti yalisababisha Serikali kutunga Sheria za kuanzisha Tume za utumishi kwa kuweka masharti na hali bora za ajira miongoni mwa waajiri tofauti wa watumishi wa Serikali ama Waajiri katika Utumishi wa Umma.

 

Tume hizo zilizoanzishwa na sheria hizo ni Tume ya Utumishi Serikalini kwa Sheria Na. 16 ya mwaka 1962 na baadaye kurekebishwa mwaka 1989, Tume ya Utumishi wa Serikali za Mitaa kwa Notisi Na. 299 iliyofutwa mwaka 1972 kwa Sheria Na.27 na kuanzishwa tena mwaka 1982 kwa Sheria Na.10 ya Serikali za Mitaa, na Tume ya Utumishi wa Walimu kwa Sheria Na.6 ya mwaka 1962 Unified Teaching Service (UTS) na mwaka 1989 kwa Sheria Na.1, kuhusu Tume ya Utumishi wa Walimu.Tume hizi zilikoma tarehe 1/07/2004 baada Makamishna wa kwanza kuteuliwa na Tume ya Utumishi wa Umma kuanza kutekeleza majukumu yake ambayo kimsingi, awali yalitekeleza na Tume hizo tatu.

 

Tume ya Utumishi wa Umma ilianzishwa mwaka 2004 kwa Kifungu 9(1) cha  Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298. Ni chombo rekebu chenye wajibu wa kuhakikisha kuwa masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma yanaendeshwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo. Tume ni Mamlaka ya Rufaa kwa Watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na maamuzi yaliyotolewa na Mamlaka zao za Nidhamu.

Ili kuhakikisha malengo ya kuimarisha Utawala Bora yanafikiwa, Tume hupokea na kutolea uamuzi rufaa na malalamiko ya watumishi wa Umma na kufanya ukaguzi wa Uzingatiaji wa Masuala ya Rasilimali Watu kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu katika Utumishi wa Umma. Aidha, huwajengea uwezo wadau wake ili waweze kutafsiri na kutekeleza ipasavyo Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma.

Kimuundo, Tume inaundwa na Mwenyekiti na Wajumbe wasiozidi sita (6) ambao wote huteuliwa na Rais. Kwa mujibu wa Sheria hiyo Tume imepewa majukumu ya kusimamia na kuhakikisha kuwa Waajiri Mamlaka za Ajira na Nidhamu katika Utumishi wa Umma wanasimamia Rasilimali Watu kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

 

Tume ya Utumishi wa Umma ambayo ni Tume rekebu inashughulikia watumishi wa Umma wa makundi ya Utumishi katika Serikali Kuu, Utumishi wa Serikali za Mitaa, Utumishi wa Afya, Utumishi wa Wakala za Serikali na Utumishi wa Taasisi na Utumishi wa Huduma za Kawaida. 

Masuala ya msingi yanayoshughulikiwa na Tume ni pamoja na: -

(i)   Kushughulikia Rufaa na Malalamiko ya Watumishi;

  (ii)   Kuelimisha Wadau jinsi ya kutekeleza Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma;

(iii)   Kufanya ukaguzi wa Rasilimali Watu kwa Taasisi zote katika Utumishi wa Umma; na

(iv)   Kuandaa Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Tume inayowasilishwa kwa Rais na Waziri mwenye dhamana na Utumishi wa Umma na Taarifa za Utekelezaji wa Majukumu ya kila Robo amabazo huwasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi.

 

 

HISTORIA YA TUME YA UTUMISHI WA UMMA.pdf

Taarifa Kwa Vyombo vya Habari

31-05-2022

TAARIFA KWA UMMA

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.