Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

TUME YA UTUMISHI WA UMMA INASISITIZA NA KUWAKUMBUSHA WATUMISHI WA UMMA KUZINGATIA YAFUATAYO

Kwa kuzingatia Tathmini ya Hali ya Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 2018 hadi Juni 2021;  Taarifa za Utekelezaji wa Masuala ya Kiutumishi kutoka kwa Waajiri, Ushughulikiaji wa Rufaa na Malalamiko ya Watumishi pamoja na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Taasisi za Umma. Tume ya Utumishi wa Umma inasisitiza na kuwakumbusha Watumishi wa Umma kuzingatia yafuatayo:-

1.0  Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Uendeshaji katika Utumishi wa Umma.
Hali halisi ya Utumishi wa Umma inaonesha kuwa bado kuna ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu unaofanywa na baadhi ya Waajiri na Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu pamoja na Watumishi wenyewe. Ukiukwaji huu unatokana na mamlaka zenye dhamana na watumishi kutozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma.
a)  Masuala ya Ajira
i)  Kuzingatia muda uliowekwa kisheria katika kushughulikia masuala ya ajira kama vile kupandishwa cheo, kuthibitisha na likizo kwa watumishi.
ii)  Kuwapandisha watumishi vyeo kwa kuzingatia sifa  kama vile utendaji kazi (OPRAS), sifa za kimuundo na Tange.
iii)  Kulipa stahili za watumishi ipasavyo kama vile gharama za likizo, gharama za matibabu na kutowarekebishia mishahara kwa wakati.


b)  Mashauri ya nidhamu
i)  Kuanzisha mashtaka kwa wakati kwa mujibu wa Sheria kwa mfano kosa la utoro mtumishi anatakiwa afunguliwe mashtaka baada ya kutoripoti kazini siku tano (5).  Baadhi za Mamlaka huanzisha mashtaka baada ya mtumishi kutoonekana kazini zaidi ya siku 100.
ii)  Kufuatwa kwa taratibu katika kuanzisha mashtaka ya nidhamu kwa mfano Maafisa ambao si Mamlaka za Nidhamu kusaini Hati za Mashtaka.
iii)  Kuwafungulia watumishi mashtaka ya nidhamu kwa makosa yale yale yaliyotolewa uamuzi na mahakama.
iv)  Hati ya mashtaka kuonyesha kwa ufasaha shtaka, vifungu au kanuni zilizokiukwa na kutokutoa muda wa kutosha  kwa mtuhumiwa kujitetea.
v)  Kuteua Kamati za Uchunguzi pale ambapo mtumishi hakukiri kosa.
vi)  Barua ya uamuzi isijumuishe makosa ambayo hayamo kwenye hati ya mashtaka ambayo hayakuchunguzwa na Kamati ya Uchunguzi. Aidha, barua ya uamuzi imjulishe mtumishi haki yake ya kukata rufaa.

2.0  Kuwa na mwitikio hasi kuhusu majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma
i)  Baadhi ya Wakala wa Serikali kutopenda kukaguliwa na Tume kuhusiana na masuala ya kiutumishi;
ii)  Baadhi ya Wakala wa Serikali kuwa na mkanganyiko katika kutumia ya Sheria ya Wakala Na. 30 ya mwaka 1997, Sheria iliyoanzisha Wakala husika, Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (Marejeo ya 2019) na Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na.6 ya mwaka 2004.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 31 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (Marejeo ya 2019), Kifungu hicho kimeweka wazi kuwa, watumishi wa Wakala na wale wa Taasisi za Umma pamoja na kutawaliwa na Sheria zilizounda Taasisi au Wakala hizo, watatawaliwa pia na Sheria ya Utumishi wa Umma kama  Kuu. Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 34A cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (Marejo ya 2019) inaelekeza kuwa endapo kutakuwa na mgongano  kati ya Sheria hizo na Sheria ya Utumishi wa Umma katika masuala ya kiutumishi, Sheria ya Utumishi wa Umma ndiyo itakayotumika.

3.0  Utunzaji usioridhisha wa kumbukumbu
Utunzaji wa kumbukumbu kwa  baadhi ya Wakala bado hauridhishi. Kutokuwepo kwa kumbukumbu sahihi husababisha Mamlaka husika kushughulikia sehemu tu ya watumishi na sehemu nyingine kutokushughulikiwa. Ni kutokana na hali hii, watumishi wa umma ambao hawajashughulikiwa hupeleka malalamiko yao kwenye Mamlaka za juu kwa kuwa wanaona hawatendewi haki na waajiri.   

4.0  Kutokuwasilisha Taarifa za utekelezaji Tume
Baadhi ya Waajiri hawawasilishi taarifa za kiutekelezaji kwa wakati au kutowasilisha kabisa jambo ambalo linakwamisha utekelezaji wa shughuli za Tume.

 5.0  Kutozingatia Maadili ya Utumishi wa Umma
 (a)  Kutokujibu barua za watumishi
i)  Baadhi ya waajiri hawajibu kwa wakati au hawajibu kabisa barua za Watumishi kuhusiana na maombi/madai yaliyowasilishwa kwao.  Hali hiyo ya kutojibiwa kwa barua inasababisha Watumishi kudhani kuwa maombi/madai yao yamekubaliwa.  Athari zake ni kuwa baadhi ya watumishi hao hufukuzwa kazi mfano kwa kosa la utoro kwa wale walioamua kwenda kusoma kwenye Taasisi mbalimbali za mafunzo bila kujibiwa barua za maombi ya ruhusa.
ii)  Baadhi ya malalamiko yanayowasilishwa Tume na watumishi wa Umma yanasababishwa na waajiri kutojibu barua na kuwapa mrejesho wa maombi/madai yao kwa wakati.

c)  Kutokuzingatia maagizo ya Tume
i)  Baadhi ya waajiri na Mamlaka za Nidhamu kuchelewa au kutotekeleza kabisa maagizo ya Tume.
ii)  Baadhi ya Waajiri na Mamlaka za Nidhamu kuchelewa kuwasilisha vielelezo vinavyohusiana na rufaa / malalamiko yaliyowasilishwa Tume.

WITO WA TUME KWA WAAJIRI, MAMLAKA ZA AJIRA, MAMLAKA ZA NIDHAMU NA WATUMISHI
i)  Kusimamia na kutekeleza kikamilifu Sheria, Kanuni na Taratibu zinazohusu masuala ya Rasilimali Watu.
ii)  Kuboresha Mifumo ya Utunzaji wa Kumbukumbu za watumishi ili waweze kufanya maamuzi sahihi na kuwahudumia vyema watumishi wao.
iii)  Kuwasilisha taarifa Tume kwa wakati na kwa kuzingatia Mwongozo wa Tume wa kuwasilisha taarifa mbalimbali zinazotakiwa kwa maamuzi.
iv)  Kuwapatia mafunzo Watendaji na watumishi walio chini yao ili waweze kuzifahamu Sheria, Kanuni na Taratibu za kiutumishi ili kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria.
v)  Kuandaa na kuhakikisha kuwa Mfumo wa Upimaji wa Wazi wa Utendaji kazi (OPRAS) unatekelezwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.
vi)  Kusimamia na kuzingatia kwa ukamilifu maadili ya kazi
vii)  Waajiri kuendesha vikao vya kazi na watumishi ili kuboresha utendaji kazi wao pamoja na kujenga umoja. 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.