Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Ukaguzi
Ukaguzi

 

HUDUMA ZINAZOTOLEWA NA IDARA YA UZINGATIAJI NA UKAGUZI WA RASILIMALI WATU

Kifungu cha 10 (1) (c) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 kimeipa Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma mamlaka ya  kufanya Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Usimamizi wa Utumishi wa Umma kwenye Wizara zote, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali; Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Taasisi na Mashirika ya Umma. Tume hufanya kazi hiyo ya Ukaguzi chini ya uratibu na usimamizi wa Idara ya Uzingatiaji na Ukaguzi wa Rasilimaliwatu inayoongozwa na Naibu Katibu.

 

Lengo kuu la kufanya Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Rasilimaliwatu ni kupima na kutathmini endapo Taasisi za Serikali zinausimamia Utumishi wa Umma kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayotolewa mara kwa mara.

Kuna Kaguzi za aina mbili zinazofanywa na Tume, Kaguzi hizo ni Ukaguzi wa Kawaida na Ukaguzi Maalum. Ukaguzi wa Kawaida hufanywa kwa kuzingatia Mpango Kazi wa Mwaka ambao hutokana na Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Tume. Taasisi zinazokaguliwa kila mwaka ni kati ya 150 hadi 180.

Aidha, Ukaguzi Maalum unaweza kutokana na Ukaguzi wa Kawaida, maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa Serikali, Maombi kutoka kwenye Taasisi, maelekezo kutoka kwa Makamishna wa Tume yanayotokana na masuala wanayoyabaini wakati wanapokuwa wanafanya uamuzi wa rufaa na malalamiko ya watumishi yaliyowasilishwa kwao na watumishi ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na Mamlaka zao za Ajira na Nidhamu.

Tume imeanza kutekeleza Mfumo mpya wa TEHAMA ambao umeundwa na Wataalam wa TEHAMA wa ndani kwa kushirikiana na Wataalam wa TEHAMA wa nje ya Tume kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali. Mfumo huo unajulikana kama “Public Service Commission Management Information Systems (PSCMIS)” ambao una moduli mbili na kati ya moduli hizo moja inatumika katika Ukaguzi wa Rasilimali Watu.

Katika utekelezaji wa Ukaguzi wa Rasilimaliwatu, Tume hutumia alama na viwango vya uzingatiaji vilivyowekwa ili kutathmini viwango vya uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika kusimamia Utumishi wa Umma. Alama hupatikana kwa kuangalia kuzingatiwa au kutozingatiwa kwa masuala mbalimbali ya Rasilimaliwatu au ya Kiutawala katika maeneo yanayokaguliwa. Maeneo yanayokaguliwa ni kama Taratibu za Ajira Mpya, Taratibu za Upandishwaji Vyeo, Mafunzo na Maendeleo ya Watumishi, Taratibu za Uendeshaji wa Mashauri ya Nidhamu, Uzingatiaji wa Maadili na Ushughulikiaji wa Malalamiko, Ushughulikiaji wa Masuala ya Anuai za Jamii katika maeneo ya kazi, Usimamiaji wa Likizo (Likizo ya Mwaka; Likizo ya Masomo; Likizo Bila Malipo; Likizo ya Uzazi; Likizo ya Kustaafu na Likizo ya Ugonjwa), Fidia ya Ajali na Magonjwa Yatokanayo na Kazi na Mafao ya Hitimisho la Ajira, na Taratibu za Ofisi, Utunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka. Kiwango cha juu cha Uzingatiaji ni kati ya asilimia 75 hadi 100; kikifuatiwa na asilimia 50 hadi 74; 25 hadi 49 na asilimia 0 hadi 24. Alama na Viwango vya uzingatiaji ni kama vilivyooneshwa katika Jedwali hapa chini:-

 

 

Jedwali Na. 1: Alama na Viwango vya uzingatiaji katika Ukaguzi wa Rasilimaliwatu

Na.

Alama

Kiwango

1.

75 – 100

Juu

2.

50 – 74

Kati

3.

25 – 49

Chini

4.

0 – 24

Hafifu


Baada ya Ukaguzi Idara ya Uzingatiaji na Ukaguzi wa Rasilimaliwatu huandaa Taarifa ya Ukaguzi ambayo hutokana na matokeo ya uzingatiaji yaliyopatikana kutoka kwa Wakaguzi. Taarifa za Ukaguzi huwa zina mapendekezo yanayopaswa kutekelezwa ili kuboresha uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika Utumishi wa Umma.

Kuna aina tatu za Taarifa za Ukaguzi zinazochakatwa na kuandaliwa na Ofisi ya Rais – Tume ya Utumishi wa Umma . Taarifa hizo ni:-

  • Taarifa za Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria kwa Taasisi moja moja zilizokaguliwa;
  • Taarifa ya Jumla ya Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria kwa Taasisi zilizokaguliwa; na
  • Taarifa za Ukaguzi Maalum.

 

Taarifa za Ukaguzi huwa zinawasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Rais,  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi ya Msajili wa Hazina na Taasisi zilizokaguliwa.