Rufaa na Malalamiko

USHUGHULIKIAJI WA RUFAA NA MALALAMIKO
1. UTANGULIZI
Tume ya Utumishi wa Umma ni chombo Rekebu kilichoundwa chini ya Kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 [Marejeo ya mwaka 2019]. Majukumu ya Tume yameanishwa katika Kifungu cha 10(1) cha Sheria hiyo. Miongoni mwa majukumu hayo ni pamoja na kupokea na kushughulikia rufaa za Watumishi wa Umma kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 [Marejeo ya Mwaka 2019]. Hivyo, Kwa mujibu wa Kifungu cha 25(1)(b) cha Sheria hiyo, Tume ni Mamlaka ya Kwanza ya Rufaa kwa Watumishi wa Umma ambao hawakuridhiki na uamuzi uliofanywa na Mamlaka zao za Nidhamu katika Utumishi wa Umma.
Aidha, Kanuni ya 73(1)(b) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022, imeipa Tume ya Utumishi wa Umma uwezo wa kushughulikia malalamiko ya Watumishi wa Umma ambao hawakuridhiki na uamuzi uliofanywa na Waajiri na Mamlaka za Ajira katika Utumishi wa Umma kuhusu masuala ya kiutumishi yanayowahusu.
2.0 MCHAKATO WA USHUGHULIKIAJI WA RUFAA NA MALALAMIKO
Tume katika kushughulikia rufaa na malalamiko hufuata hatua zifuatazo:-
2.1 Mapokezi ya Rufaa na Malalamiko
(i) Rufaa na malalamiko hupokelewa kwa utaratibu wa kawaida wa kupokea barua au mawasiliano ya Serikali kwa kugongwa mhuri tarehe iliyopokelewa.
(ii) Kujiridhisha kuona iwapo kuna barua ya uamuzi unaopingwa na vielelezo ambavyo Mrufani/Mlalamikaji ametumia kujenga au kuthibitisha hoja za rufaa yake.
(iii) Husajiliwa kwa kupewa namba ya usajili (Track Number) ambayo Mrufani au Mlalamikaji huitumia katika kufuatilia kujua ‘status’ ya suala lake.
(iv) Kukiri mapokezi ya rufaa au malalamiko kwa Mrufani au Mlalamikiwa na kujulishwa namba ya usajili (Track Number) aliyopewa.
(v) Mamlaka ya Nidhamu ya Mrufani hujulishwa mapokezi ya rufaa husika na kutakiwa kuwasilisha vielelezo vyote vilivyotumika katika kufikia uamuzi dhidi ya Mrufani ndani ya siku kumi na nne (14) tangu kupokea barua ya Tume. Baadhi ya vielelezo muhimu ambavyo hutakiwa ni pamoja na:-
- Hati ya Mashtaka na Notisi.
- Barua ya utetezi wa Mrufani dhidi ya tuhuma aliyopewa/alizopewa.
- Barua za uteuzi wa Wajumbe wa Kamati ya Uchunguzi.
- Hadidu za Rejea zilizotumiwa na Kamati ya Uchunguzi.
- Barua ya kukabidhi mwenendo na Taarifa ya Kamati ya Uchunguzi.
- Taarifa ya Kamati ya Uchunguzi na Mwenendo wa Shauri;
- Muhtasari wa Kikao cha Mamlaka ya Nidhamu iliyotoa uamuzi (Mamlaka za Serikali za Mitaa au Bodi ya Wakurugenzi).
- Barua ya uamuzi.
- Maelezo ya Mamlaka ya Nidhamu kuhusiana na rufaa husika yakiwemo majibu ya hoja za Mrufani.
- Taarifa au maelezo binafsi (CV).
- Rejesta au ‘Dispatch’ zilizotumika kufanya mawasiliano na Mrufani wakati wote wa mchakato wa shauri la nidhamu.
- Kielelezo chochote muhimu kilichotumiwa na Mamlaka ya Nidhamu katika kufikia uamuzi wa shauri husika.
(vi) Kwa upande wa malalamiko, Mwajiri wa Mlalamikaji kuhusu Tume kupokea malalamiko husika na kutakiwa kuwasilisha maelezo na vielelezo vyote vilivyotumika katika kufikia uamuzi dhidi ya Mlalamikaji ndani ya siku kumi na nne (14) tangu kupokea barua ya Tume.
2.2 Uchambuzi na uamuzi wa Tume
Tume kwa mujibu wa Kanuni ya 62(3) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, inatakiwa kufanya uchambuzi wa rufaa na kufanya uamuzi wake ndani ya siku 90 baada ya kupokea vielelezo kutoka kwa mamlaka ya Nidhamu.
Aidha, Kanuni ya 61(4) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, imeipa Tume mamlaka ya kuendelea na uchambuzi wa rufaa kwa kutumia vielelezo vya upande mmoja pale ambapo Mamlaka ya Nidhamu itashindwa kuwasilisha vielelezo husika ndani ya siku 14 tangu ilipopokea maagizo ya Tume bila kutoa sababu za msingi.
2.3 Mrufani/Mlalamikaji kupewa uamuzi wa Tume
Baada ya Tume kufanya uamuzi wake, Mrufani/Mlalamikaji anatakiwa kupata uamuzi wa Tume ndani ya siku 21 baada ya Mkutano wa Tume uliofanya uamuzi wake kukamilika. Aidha, Warufaniwa na Walalamikiwa pia hujulishwa kuhusu uamuzi wa Tume.
2.4 Haki ya kukata rufaa
Endapo Mrufani na Mrufaniwa hawakuridhika na uamuzi wa Tume kwa mujibu Kanuni ya 61(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022 wanayo haki ya kukata rufaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya siku 45 tangu tarehe ya kupokea uamuzi wa Tume.
HITIMISHO
Ili Tume iweze kushughulikia rufaa na malalamiko ya Watumishi wa Umma kwa wakati, ni wajibu wa Watumishi, Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu katika Utumishi wa Umma kutimiza wajibu wao kuhakikisha kuwa Tume inawezeshwa kupata taarifa zote muhimu kwa ajili ya uchambuzi na hatimaye kufanya uamuzi wa masuala hayo kwa wakati.