Tume ya Utumishi wa Umma kushughulikia Rufaa na Malalamiko
Na Hajra Hashim, Dodoma.
Tume ya Utumishi wa Umma inatarajia kufanya Mkutano wa Kwanza wa Tume kwa ajili ya kushughulikia Rufaa na Malalamiko ya Watumishi wa Umma kuanzia tarehe 21 Septemba hadi 16 Oktoba 2026 katika Ofisi za Tume zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 18,2026 Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Nolasco Kipanda amesema kuwa Mkutano huo utajadili na kushughulikia Rufaa na Malalamiko mbalimbali yaliyowasilishwa mbele ya Tume, pamoja na masuala mengine yanayohusiana na utekelezaji wa majukumu ya Tume.
Aidha, Katibu huyo ameeleza kuwa Tume imehamia katika Jengo la Serikali lililopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, ambapo Ofisi za Tume sasa zinaendelea na shughuli zake katika eneo hilo.
Hatua hiyo inalenga kuwezesha Tume kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutoa huduma kwa wadau na Watumishi wa Umma kwa kuzingatia misingi ya sheria, haki na utawala bora.
Shukran za dhati ziende kwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa Ofisi zinazokidhi mahitaji ya Watumishi wa Tume na kuweza kutekeleza wajibu wao kama ilivyokusudiwa.