Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

TATHMINI YA MPANGO MKAKATI WA TUME UTUONGOZE KUFANYA KAZI KUFIKIA MALENGO YA SERIKALI- KIRAMA

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama ameitaka Menejimenti ya Tume hiyo kwa kushirikiana na wadau wake kufanya tathmini ya kati ya Mpango Mkakati wa Tume ili uwaongoze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi kuweza kufikia malengo ya Taasisi na Serikali kwa ujumla.

Bw. Kirama amesema hayo alipokuwa akifungua kikao kazi cha tathmini ya kupitia Mpango  Mkakati  wa Tume wa mwaka 2021/2022 hadi mwaka 2025/2026 kilichofanyika Septemba 30, 2023 Jijini Dodoma.

“Tunafanya tathmini kupitia Mpango Mkakati wa mwaka 2021/22  hadi mwaka 2025/2026 na tumefikia muda wa kati. Tunafahamu kumekuwepo na mabadiliko mbalimbali ya Dira, Sera, Sheria, Majukumu ya Taasisi na pia mwelekeo wa Serikali. Kupitia kikao kazi hiki tujipime kwa kiasi gani toka tumeandaa Mpango huu wa Tatu tumefanikiwa kiasi gani katika kufikia malengo tuliyojiwekea. Tathmini hii itatusaidia kujua tumepiga hatua kiasi gani, nguvu kubwa iwekwe wapi katika kipindi kilichobaki ili Mpango huu ukamilishwe kwa ufanisi unaotakiwa.” amesema Bw. Kirama.

Bw. Kirama amefafanua na kusisitiza kuwa ni muhimu Tume kujipanga kuwa sehemu ya maono ya nchi na maboresho yanayoendelea kufanyika kuhakikisha  utumishi wa umma unatoa huduma bora zenye kukidhi matarajio ya wananchi na watumishi wa umma.

“Mpango Mkakati  utuongoze kama Dira ya Taasisi na malengo ya Serikali, wekeni malengo yenye kuleta matokeo na kubainisha changamoto na  ufumbuzi utakaopatikana hapa tulipo ili kwenda mbele zaidi. Mpango Mkakati huu utupe changamoto ya kufanya kazi kwa nidhamu na weledi zaidi kufikia matarajio ya Serikali na wadau wetu” amesema Bw. Kirama.

Akizungumza kuhusu Tume, Bw. Kirama amesema kuwa tunafahamu kwa sasa inahudumia wateja wenye uelewa mkubwa wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika  Utumishi wa Umma, wadau wanatambua haki zao, wanataka matokeo na kupata mrejesho wa haraka.

“Ni muhimu sana kuangalia tunafanya nini kwa upande wa rasilimali watu, kubadilisha fikra na namna ya kufanya kazi sambamba na kuboresha mifumo yetu ya kimenejimenti na matumizi ya TEHAMA katika kuwahudumia wadau wetu. Mambo tuliyofanya hadi kufikia kipindi cha kati cha Mkakati huu tunahitaji kujiuliza wapi tuboreshe zaidi. Tufanye nini kuhakikisha tunatoa huduma bora zaidi, hususan katika kushughulikia rufaa na malalamiko yanayowasilishwa Tume na kuongeza ubora wa namna tunavyoshughulikia jukumu letu la Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma” ameongeza Bw. Kirama.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kitengo cha Mipango, Ufuatiliaji na  Tathmini kutoka Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Abdallah Mvungi amesema  lengo la Kikao kazi hiki ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tume kwa kipindi cha Kati, ambao ndio dira kuelekea mafanikio na maendeleo endelevu. Aliongeza kusema kuwa mapitio hayo ya Mpango na Mikakati ya kuutekeleza yatawashirikisha pia wadau muhimu ili kupata maoni yao kwa lengo la kuboresha.

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.