Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Tume ya Utumishi wa Umma yabainisha Mafanikio ya Miaka Mitatu
17 Apr, 2025
Tume ya Utumishi wa Umma yabainisha Mafanikio ya Miaka Mitatu

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. John Mbisso ametoa shukrani za dhati kwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Mhe.Jaji (Mst) Hamisa H.Kalombola pamoja na Makamishna 6 kwa kutekeleza mambo makubwa muhimu tangu walipoteuliwa Aprili 11,2022 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Katika hafla iliyofanyika  Aprili 11,2025 katika Ukumbi wa UCSAF Jijini Dodoma ya kuwaaga Viongozi hao baada ya kumaliza muda wao  mara baada ya Mkutano maalumu wa kushughulikia Rufaa na Malalamiko ulioendeshwa kwa Siku mbili kuanzia Aprili 10,2025 hadi Aprili 11,2025.

Bw. Mbisso amesema kuwa Viongozi hao wamefanikisha utekelezaji wa majukumu ya Tume ikiwemo Uamuzi wa Rufaa 1,879 sawa na Asilimia  97.3  ya Rufaa 1,932 zilizokuwepo, ambapo ni sawa na ongezeko la Asilimia   117.8  ukilinganisha na Awamu iliyopita iliyoshughulikia Rufaa 887.

Aidha, Tume hiyo imefanikisha kuimarisha Ukaguzi wa uzingatiaji wa Sheria kwa kuongeza Idadi ya Taasisi zilizokaguliwa kwa Asilimia 50 Kutoka Taasisi 110 mwaka 2021/2022 hadi Taasisi kati ya 160 hadi 180 mwaka 2024/2025.

Tume imefanikisha Utoaji na Usambazaji wa Miongozo ili kukidhi mahitaji na mazingira ya kiutumishi kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Utumishi wa Umma, Ushirikiano wa kikanda kati ya Tume ya Utumishi wa Umma Tanzania na Tume za barani Afrika, Ukanda wa SADC .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume Jaji (Mst.) Mhe.Hamisa H. Kalombola amezipokea shukrani hizo kwa niaba ya Makamishna na kusema kuwa Mafanikio hayo yaliyopatikana si kwa juhudi zao pekee bali  ushirikiano mkubwa walioupata kutoka kwa Watumishi wa Tume hiyo . “Mafanikio haya hayakuja kwa bahati mbaya bali ni umoja na Ushirikiano kati ya Makamishna na Sekretarieti kuanzia ngazi ya chini mpaka ngazi ya juu kwa kila Idara na Kitengo, Tunaomba tamaduni hii iendelee hata kwa watakaokuja ili kufanikisha malengo ya Serikali yaliyokusudiwa “ Amesema Mhe. Kalombola.