Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA ZIMESISITIZWA KUSHUGHULIKIA MASUALA YA RASILIMALI WATU KATIKA UTUMISHI WA UMMA KWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU

  

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Elikana Balandya amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha masuala ya usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma yanatekelezwa kikamilifu katika ngazi zote kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.

Bwana Balandya amesema hayo Jijini Mwanza wakati akifungua kikao kazi kati ya Tume ya Utumishi wa Umma na washiriki kutoka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichoandaliwa ili kuwajengea washiriki uwezo wa kuzielewa, kutafsiri na kusimamia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazoongoza Utumishi wa Umma kwa lengo la kuhakikisha kwamba Utumishi wa Umma katika ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa unazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

“Nachukua fursa hii kuzikumbusha Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa  zinapaswa kuwa makini na kusimamia ipasavyo Sheria zinazowaongoza katika utekelezaji wa majukumu yao. Tunatambua kuwa Sheria, Kanuni na Taratibu zinapokiukwa Serikali inapata hasara. Serikali inapata hasara kwa kuingia gharama ya kulipa fidia lakini hasara pia pale inapotumia fedha kurejea mashauri ambayo yaliendeshwa bila kufuata Sheria, kama kungekuwa na uzingatiaji fedha hizi zingeweza kutumika kwa shughuli za kuleta maendeleo. Natoa rai kwa Mamlaka za Mitaa kuhakikisha masuala ya usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma yanatekelezwa kikamilifu katika ngazi zote kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa” alisema Bwana Balandya.

Akizungumza kuhusu majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma alisema, Tume pamoja na majukumu mengine ina wajibu wa kushuhughulikia rufaa za watumishi wanaopinga uamuzi wa Mamlaka zao za Nidhamu. Pia inashughulikia malalamiko ya watumishi wa umma dhidi ya Mamlaka zao za Ajira. Alisema kuwa, Tume katika utekelezaji wa jukumu hili, imebaini kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ndizo zinaongoza kwa kutozingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma wakati wa kushughulikia masuala ya watumishi yakiwemo mashauri ya nidhamu na hivyo kusababisha mashauri mengi yanayowasilishwa Tume kurudishwa ili yakaanze upya hivyo kuisababishia Serikali hasara.

Kwa upande wa baadhi ya Mamlaka za Nidhamu na Mamlaka za Ajira kutotekeleza maagizo ya Tume, alizikumbusha Mamlaka hizo kwa kusema kuwa zinapaswa kutambua kuwa kutotekeleza maagizo ya Tume ni ukiukwaji wa Sheria na muhimu watambue kwamba wanapokuwa hawaridhiki na maagizo ya Tume wanayo haki ya kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais.

Kwa upande wa jukumu la ukaguzi alisema, Tume ya Utumishi wa Umma imepewa Mamlaka ya kufanya Ukaguzi wa uzingatiaji katika Taasisi zote za Umma  kwa lengo la kuimarisha uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na Taasisi za Umma ili kuongeza tija kwenye utendaji wa Serikali na kuwa na matumizi sahihi ya Rasilimali Watu.

“Nachukua nafasi hii kuwaomba washiriki kujenga mahusiano na mashirikiano mazuri na Tume ili kupitia Mkakati wake iliojiwekea wa kuzijengea uwezo Wizara, Idara za Serikali, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa, Manispaa na Halmashauri za Wilaya, muwe ni wanufaika wa kwanza wa uelimishwaji kuhusu masuala ya uzingatiaji wa Sheria, hivyo msikae kusubiri na kungoja hadi pale mtakapofikiwa na Tume wakati wa zoezi la ukaguzi” alisema.

Akizungumza kuhusu Taarifa zinazotolewa na Tume alisema zinaonyesha kuwa miongoni mwa makosa yanayosababisha watumishi kuchukuliwa hatua ni utoro kazini, wizi, ubadhirifu, rushwa, uzembe, uhujumu uchumi na mengine.

Bwana Balandya amehitimisha kwa kuwakumbusha Waheshimiwa Wenyeviti kuwa kupitia Mabaraza ya Madiwani ambayo wao ni Mamlaka ya Nidhamu kwa Watumishi wa Umma watambue wanapaswa kuhakikisha wakati wote wanatoa uamuzi wa haki bila upendeleo wowote.

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.