Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

MUHOJI AFUNGUA KIKAO KAZI KATI YA TUME NA WADAU KUJADILI MPANGO MKAKATI WA MWAKA 2021/22 – 2025/26

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bwana Nyakimura Muhoji  leo amefungua Kikao Kazi kinachofanyika Mkoani Morogoro kati ya  Tume  na Wadau kujadili Mpango Mkakati  mpya wa Tume wa  mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026 ulioandaliwa  baada ya kuhuisha Mpango Mkakati uliokuwepo awali wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21.
Muhoji amesema kuwa majukumu yaliyo kasimiwa kwa Tume ya Utumishi wa Umma ndiyo yanaipa Tume uhalali wa kuwa na Mpango Mkakati huu ulioandaliwa. Amewakumbusha washiriki kuwa kazi kubwa ya Tume ni kuhakikisha kwamba katika Utumishi wa Umma panakuwepo na Uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia uendeshaji wa masuala ya Rasilimali Watu.
“Majukumu haya yameainishwa katika Kifungu cha 10(1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 (Marejeo ya mwaka 2019). Baadhi ya Majukumu haya ni:- Kutoa Miongozo na kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma; Kupokea na kushughulikia malalamiko ya watumishi  na rufaa za mashauri yaliyotolewa uamuzi na Mamlaka za Nidhamu; Kuwezesha, kufuatilia na kutathmini utendaji kazi wa watumishi wa Umma wa ngazi mbalimbali ili uwe wa ufanisi na wenye kuzingatia matokeo; na Kuhakikisha kuwa Taratibu za Uendeshaji za Utumishi wa makundi mbalimbali ya kiutumishi zinatayarishwa na kutumika ipasavyo” alifafanua Bw. Muhoji.
Alisema kuwa pamoja na mabadiliko ya Muundo wa Tume uliopitishwa na kuidhinishwa na Mheshimiwa Rais mwaka 2018, bado Tume iliendelea kutekeleza majukumu yake kwa kutumia Mpango Mkakati uliokuwepo. Hivyo, ushirikishaji wa wadau katika Kikao kazi hiki ni moja ya hatua muhimu katika uandaaji wa Mpango Mkakati, maana  Wadau ni jicho lingine la Tume kwa kuwa sote tunafahamu kuwa hatuwezi kujitathmini wenyewe tukapata kitu bora bila kumshirikisha yule tunayemhudumia, tunafahamu pia  kuwa upo mchango kutoka kwa wadau wetu katika kuuboresha Mpango Mkakati huu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji, Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. David Pwele alisema Tume imeandaa kikao kazi hiki kwa lengo la kujadili, kufanya tathmini na  kujiridhisha kama Mpango Mkakati huu umegusa vya kutosha huduma inazozitoa kwa wadau wake kupitia majukumu ya Tume ambayo imepewa kwa mujibu wa Sheria.

Imeandaliwa na:-
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
TUME YA UTUMISHI WA UMMA
MOROGORO  

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.