Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

JAJI (MST.) DKT. BWANA:- SERIKALI IMEFANYA KAZI KUBWA KUSIMAMIA NIDHAMU YA UTUMISHI WA UMMA

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji (Mstaafu) Mheshimiwa Dkt. Steven James Bwana, amesema Serikali imefanya kazi na  juhudi kubwa  kuhakikisha Watumishi wa Umma nchini wanafanya kazi kwa weledi, kwa kuzingatia maadili, sheria, kanuni na taratibu.
Dkt. Bwana amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Utumishi wa Umma.
“Serikali imefanya kazi kubwa ya kuongeza uwajibikaji na kusimamia nidhamu ya watumishi wa umma. Kwa upande wa Tume nimeridhika na maendeleo makubwa katika huduma zitolewazo na Tume. Hata hivyo, ongezeni kasi zaidi ya kushughulikia  rufaa na malalamiko ya watumishi yanayowasilishwa Tume” amesema.
 Jaji Mstaafu Dkt. Bwana amesema wananchi wanahitaji kuona utendaji  wa kazi wenye kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu. Watumishi wanapaswa kutambua kuwa kuwajibika kikamilifu kunaharakisha maendeleo yanayotarajiwa na wananchi na kutoa huduma bora.
“Tume ni chombo kinachofanya kazi nyeti ya kusimamia  Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma. Hivyo, kila Idara na Kitengo ni muhimu kuwa  na mkakati endelevu wa kuboresha sehemu yake ya utoaji wa huduma. Tambueni mafanikio ya Tume ni mafanikio ya Taifa kwa ujumla. Nafahamu watumishi wa Tume mmekuwa mkijitahidi kufanya kazi zenu kwa bidii, nawashukuru kwa kujitoa kwenu katika kufanya kazi ili kufikia malengo ya Tume  licha ya changamoto zilizopo. Tutaendelea kushirikiana pamoja na Makamishna wa Tume kutatua changamoto hizo” alisema.
Katika Mkutano huo Wajumbe walipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Tume kwa mwaka 2020/ 2021 na mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2021/2022.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume, Bwana Nyakimura Muhoji alisema licha ya kuwepo kwa changamoto kama ucheleweshaji wa vielelezo vya rufaa na malalamiko, kuchelewa au kutowasilishwa kwa taarifa za hali ya utumishi, Tume imeweza kutekeleza majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kuandaa Taarifa ya Hali ya Utumishi wa Umma Nchini kwa mwaka 2019/20 na kuiwasilisha  kwa Mh. Rais na taarifa za robo ya kwanza na ya pili katika mwaka wa fedha 2020/21 zilizowasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi. Taarifa hizi zinamsaidia Rais na Katibu Mkuu Kiongozi kufahamu hali ya usimamizi wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma.
“Tume imeweza kufanya Ukaguzi wa Kawaida katika Taasisi za Umma ambapo mpaka mwezi Machi 2021 ukaguzi katika Taasisi 86 umefanyika. Tume imetoa maamuzi ya rufaa 227 na Malalamiko 67 na  elimu kwa wadau imeendelea kutolewa kuhusu utekelezaji wa Sheria katika masuala ya Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma” alisema.
Katika kikao hicho cha Baraza la Wafanyakazi, miongoni mwa shughuli zilizofanyika ni pamoja na  uchaguzi wa Katibu wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume, ambapo Bwana Robert Lwanji alichaguliwa na Wajumbe kushika nafasi hiyo.

____________________

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.