Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

MAMLAKA ZA AJIRA NA NIDHAMU ZATAKIWA KUHITIMISHA KWA WAKATI MASHAURI YA WATUMISHI WANAOKARIBIA KUSTAAFU

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Balozi (Mstaafu) Daniel Ole Njoolay, ametoa wito kwa Mamlaka za Nidhamu na Waajiri kuhakikisha wanahitimisha kwa wakati mashauri ya nidhamu yanayowakabili  watumishi wa umma wanaokaribia kustaafu ili watakaothibitika kuwa hawakutenda makosa wapate haki zao kwa wakati na wastaafu kwa heshima.

Mheshimiwa Balozi (Mstaafu) Njoolay alisema hayo wakati wa Kikao cha 15 cha Mkutano wa Pili wa Tume kwa mwaka wa fedha 2020/2021 uliomalizika mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam.

“Bado kuna ujanja ujanja unatumiwa na baadhi ya Mamlaka za Nidhamu kwa kuchelewesha kuhitimisha mashauri ya watumishi wa umma wanaokaribia kustaafu bila sababu za msingi. Mamlaka za Nidhamu zinasubiri hadi watumishi wanaotuhumiwa kutenda makosa wanastaafu. Hii si sawa, wanapaswa kutenda haki kwa kuhitimisha mashauri haya kwa wakati ili haki ionekane imetendeka na wastaafu kwa heshima” alisema Mheshimiwa Balozi (Mstaafu) Njoolay.

Kwa upande wake Kamishna wa Tume, Mheshimiwa George Yambesi, alisema Serikali imeweka na kuainisha  taratibu za kushughulikia masuala ya nidhamu kwa watumishi wa umma wanaotuhumiwa kutenda makosa. Hivyo, ni wajibu wa Mamlaka za Nidhamu na Waajiri kuhakikisha wanazingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa katika kushughulikia masuala ya nidhamu.

Mheshimiwa Yambesi alisema kuwa, “Upande wa Kamati za Uchunguzi zinazoundwa tumebaini kuwepo kwa mapungufu na makosa ya kiutendaji. Ni muhimu Kamati hizi ziundwe na wajumbe wenye sifa na zitekeleze majukumu yake kwa wakati” alisema Kamishna Yambesi.

Kamishna Yambesi, alizitaka, Mamlaka za Nidhamu kuhakikisha kuwa Kamati za Uchunguzi zinazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na kutoa taarifa zilizo makini ili haki ionekane imetendeka.

 

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.