Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

MAMLAKA ZA AJIRA NA NIDHAMU KWA WATUMISHI WA SERIKALI ZA MITAA (MABARAZA YA MADIWANI) ZINAPASWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA TARATIBU

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Jaji (Mstaafu) Dkt. Steven Bwana, ametoa wito kwa Mamlaka za Nidhamu katika Serikali za Mitaa, yaani Baraza la Madiwani, kuhakikisha wanashughulikia masuala ya nidhamu ya watumishi wa umma kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

Mheshimiwa Jaji (Mst.) Dkt. Bwana, amesema hayo Jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki wakati wa mahojiano maalum baada ya kuhitimisha Mkutano wa Tume uliofanyika kuanzia tarehe 30 Novemba 2020 hadi tarehe 18 Disemba 2020.

Mheshimiwa Dkt. Bwana alisema Waheshimiwa Madiwani wanapotoa uamuzi kuhusu masuala ya kiutumishi wanatakiwa kutofautisha  taratibu za ajira na taratibu za nidhamu. Alisema taratibu hizo haziunganishwi pamoja, ni tofauti. Hivyo, wakati wanatekeleza majukumu yao Madiwani wanatakiwa kushughulikia masuala ya watumishi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu bila kuleta mgongano wa maslahi, undugu, upendeleo na watende haki.

“Ili kufanikisha hili nitoe wito kwa Halmashauri zetu kuweka katika bajeti zao gharama za utekelezaji wa mipango ya mafunzo kwa Waheshimiwa Madiwani wao ili wapatiwe mafunzo ya kuwajengea uwezo. Tume ya Utumishi wa Umma inatoa mafunzo kuhusu usimamizi na uendeshaji wa masuala ya Rasilimali Watu. Pia kuna vyuo vya Serikali za Mtaa Hombolo na Chuo cha Utumishi wa Umma, ni muhimu Wakurugenzi wakafanya mawasiliano na Taasisi hizi” alisema Mheshimiwa Dkt. Bwana.

Katika mkutano huo Namba 2 wa mwaka 2020/2021 Tume ilitoa uamuzi wa Rufaa 150 na Malalamiko mawili (2) yaliyowasilishwa na Watumishi mbalimbali wa Umma.

Kati ya rufaa 150 zilizotolewa uamuzi rufaa 65 zilikataliwa; rufaa 9 zilikubaliwa; rufaa 15 zilikubaliwa kwa masharti kwamba zikashughulikiwe upya na Mamlaka zao za Nidhamu. Aidha, rufaa 61 zilikataliwa kwa kuwa ziliwasilishwa nje ya muda uliowekwa kwa mujibu wa Sheria.

Kwa upande wa malalamiko, Tume ilipokea na kutoa uamuzi wa malalamiko 2 ambapo  malalamiko  hayo  yalikubaliwa. 

Aidha, Tume ilipokea, kujadili na kupitisha Taarifa nne (4) ambazo ni Taarifa ya Utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa kipindi cha  tarehe 01 Julai 2019 hadi tarehe 30 Juni 2020. Taarifa ya Utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Robo ya Kwanza ya mwaka wa fedha 2020/2021. Taarifa ya Ukaguzi wa Uzingatiaji wa Sheria katika usimamizi wa Rasilimali Watu katika Taasisi 77 kwa mwaka wa Fedha 2019/2020 na Taarifa ya Ukaguzi maalum wa masuala ya uendeshaji wa Rasilimali watu  uliofanyika mwezi Agosti 2020 katika Mamlaka moja Jijini Dar es Salaam.

 

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.