Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

MUHOJI: Azindua Kamati Tendaji ya TEHAMA "ICT Steering Committee" ya Tume ya Utumishi wa Umma

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji (pichani) amezindua Kamati Tendaji ya TEHAMA “ICT Steering Committee” ya Tume na kuiagiza itekeleze majukumu yake ipasavyo.

Bw. Muhoji amesema hayo wakati wa Kikao cha Kwanza cha Kamati Tendaji ya TEHAMA ya Tume kilichofanyika mwanzoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na ajenda zilizowasilishwa na kujadiliwa, aliizindua Kamati hiyo na kuwaagiza Wajumbe wa Kamati kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao  kikamilifu.


“Kamati hii Tendaji ya TEHAMA ni chombo ambacho kilikuwa hakijaanzishwa ndani ya Taasisi yetu. Baada ya kuwa imetungwa Sheria ya Serikali Mtandao Na.10 ya mwaka 2019, kila Taasisi ya Umma inatakiwa kuwa na Kamati hii ya ICT Steering Committee  na sisi Tume ni miongoni mwa wadau, tumeamua kuianzisha na leo tunaizindua Kamati hii. Nafahamu mna majukumu mengine ndani ya Taasisi  yetu, mmepatiwa pia jukumu hili, hakikisheni mnasimamia utekelezaji wa majukumu yenu ya Kamati Tendaji ya TEHAMA ambayo yameainishwa ndani ya Sheria hii ipasavyo” alisema.

Katika Kikao hiki, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Sylvester Koko,  aliwasilisha mada kuhusu Sera ya TEHAMA ya Tume ambayo imeandaliwa na alisema,  Sera hii  itatuongoza nini tufanye Tume na kwa namna gani masuala ya TEHAMA na itatolewa kwa watumishi wanaotumia mifumo, ili iweze kutumika wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Bw. Koko aliwasilisha pia Mpango wa Kujikinga na Majanga ya Kimtandao ulioandaliwa na Tume na Muongozo wa Uendeshaji wa Kamati Tendaji za TEHAMA katika Taasisi za Umma uliotolewa na Mamlaka ya Serikali Mtandao ”eGA”.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma ya Sheria wa Tume,  Bw. Charles Mulamula  alisema miongoni mwa majukumu ya Kamati hii inayoundwa na Wajumbe wasiopungua 6 na wasiozidi 7 ni kutoa ushauri wa kitaalam kwa Mkuu wa Taasisi na Kusimamia utekelezaji wa Serikali Mtandao katika Taasisi, ikiwa ni pamoja na Miundombinu; Usimamizi wa TEHAMA na Data.

Akizungumzia kuhusu “e- Government Services” , Bw. Mulamula alisema utaratibu wa matumizi ya data na mtandao lazima yaendane na matakwa ya Sheria ya Nchi.

Kamati Tendaji ya TEHAMA ya Tume ya Utumishi wa Umma inaongozwa na Mwenyekiti ambae ni Bw. Nyakimura M. Muhoji (Katibu wa Tume); Katibu ni Bw. Sylvester T. Koko (Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA); na Wajumbe wa Kamati ni:- Bw. John C. Mbisso (Naibu Katibu); Bw. Maurice M. Ngaka (Mhasibu Mkuu); Bw. Baraka Kipigapasi (Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani); Bw. Ernest Mbago (Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi); Bw. Musa P. Magunguli (Mkurugenzi wa Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini).

Sekretarieti ni Bw. Alex A. Mero na Bw. Justine L. Jackson (Kitengo cha TEHAMA). 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.