Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

MAFUNZO YA UKAGUZI WA RASILIMALI WATU YANATOLEWA KWA WATUMISHI WA TUME KWA LENGO LA KUWAJENGEA UWEZO

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji amesema kuwa mafunzo ya ukaguzi wa rasilimali watu yanayotolewa kwa  Watumishi wa Tume yamelenga kuwajengea uwezo ili waweze kutekeleza jukumu la msingi la ukaguzi wa rasilimali watu unaofanywa na Tume ipasavyo.

Bw. Muhoji amesema hayo hivi karibuni  Jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya wakaguzi wa masuala ya rasilimali watu  na waingiza taarifa  yaliyotolewa kwa watumishi wa Tume kwa lengo la  kuwajengea uwezo na kuwawezesha kuwa na uelewa wa pamoja.

“Lengo la mafunzo haya ya ukaguzi wa rasilimali watu ni kuwajengea uwezo na kuwawezesha kuwa na uelewa wa pamoja. Kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa na michango ya washiriki iliyotolewa, mafunzo haya yatawasaidia kujiimarisha katika utekelezaji wa jukumu lenu la ukaguzi wa kawaida wa Rasilimali watu unaotarajia kufanyika hivi karibuni, kuangalia uzingatiaji wa  Sheria, Kanuni na Taratibu” alisema.

Bw. Muhoji aliwakumbusha Watumishi wa Tume kutumia ukaguzi huu kwa kutoa elimu na kujitangaza kwa Taasisi zitakazokaguliwa ili ziweze kutambua majukumu ya msingi yanayotekelezwa na Tume ya Utumishi wa Umma.

Miongoni mwa mada zilizotolewa katika mafunzo haya ni Uandaaji wa Taarifa za Ukaguzi; Hoja za Ukaguzi na Maadili ya Utumishi wa Umma kwa watumishi watakaoshiriki ukaguzi wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma.

Tume ya Utumishi wa Umma ina jukumu la kufanya Ukaguzi wa Rasilimali Watu kwa lengo la kutathmini, kufahamu au kuona uzingatiaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika uendeshaji wa Utumishi wa Umma, unaofanywa na Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu na Watumishi wenyewe.  

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.