Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

SHERIA YA UTUMISHI WA UMMA IMEWAPA WATENDAJI WAKUU DHAMANA NA MAMLAKA YA KUSIMAMIA RASILIMALI WATU WALIO CHINI YAO


 SHERIA YA UTUMISHI WA UMMA IMEWAPA WATENDAJI WAKUU DHAMANA  NA MAMLAKA YA KUSIMAMIA RASILIMALI WATU WALIO CHINI YAO  

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, mheshimiwa Balozi (mstaafu) John Haule amesema kuwa Sheria ya Utumishi wa Umma sura ya 298, imewapa Watendaji Wakuu dhamana na Mamlaka ya kusimamia Rasilimali watu walio chini yao.

Kamishna Haule ameyasema hayo hivi karibuni katika Mikoa ya Mwanza na Simiyu kwenye mikutano iliyohudhuriwa na baadhi ya Wakuu wa Wilaya, Watendaji wakuu, Wakuu wa Taasisi za Umma, Wakurugenzi na watumishi wa umma iliyofanyika kwa lengo la kuwakumbusha Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu na watumishi wa umma umuhimu wa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maelekezo halali yanayotolewa na Serikali.

“Watendaji wakuu kwa mujibu wa Sheria mmepewa dhamana na Mamlaka ya kusimamia Rasilimali watu walio chini yenu katika maeneo ya Ajira, Upandishwaji vyeo, Uendelezaji wa Watumishi kwa njia ya Mafunzo, Tathmini ya Utendaji kazi ya wazi, Uchukuaji wa Hatua za Nidhamu na hitimisho la kazi kwa mujibu wa Sheria”. Alisema, pia Hakikisheni mnachukua hatua kwa wakati na stahiki pale watumishi walio chini yenu inapothibitika wametenda makosa.

Mheshimiwa Haule alifafanua kuhusu Tume inavyosimamia masuala ya Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma kuwa, Tume ina wajibu wa kuhakikisha kwamba kunakuwepo na Utawala bora katika usimamizi na uendeshaji wa Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma ili uweze kutoa matokeo yenye tija na huduma bora inayotarajiwa na wananchi. 

“Tume hutekeleza jukumu hili ambalo ni la urekebu kwa kutoa miongozo ya masuala ya Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma; Tume hufanya  ukaguzi wa Rasilimali watu  kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Taratibu, Kanuni na Miongozo ya Serikali, hupokea na kushughulikia Rufaa na Malalamiko ya watumishi wa umma wanaopinga maamuzi yanayotolewa na Mamlaka zao za Nidhamu kupitia jukumu hili Tume ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha  haki inatendeka katika masuala ya Ajira na Nidhamu. Ili kuwajengea uwezo wa kusimamia kwa ufanisi uendeshaji wa Rasilimali watu katika Utumishi wa umma Tume imeendelea kuwawezesha na kuwaelimisha wadau wake” alisema Mheshimiwa Haule.

Akizungumzia baadhi ya changamoto zilizobainishwa na Tume alisema kuwa bado kuna ukiukwaji wa Sheria katika kushughulikia masuala ya Ajira na nidhamu kunakofanywa na baadhi ya Waajiri na Mamlaka za Ajira na nidhamu na hii inasababisha kuwepo kwa rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma.

Kamishna Haule alisisitiza ni muhimu sana kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu na watumishi wote wa umma kila mmoja kwa nafasi yake atimize wajibu wake kwa kuzingatia Maadili, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa ili kuboresha utendaji wa kazi na hatimae kutoa huduma bora kwa wananchi.

                                                                          *********************

 

  

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.