Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Watumishi wa Umma watakiwa kuwa na maadili

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Jaji Mstaafu Dkt. Steven Bwana amesema bado kuna baadhi ya watumishi wa Umma ambao hawana maadili na amewataka kujirekebisha haraka.

Aidha, amewataka watumishi wa Umma kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa wakati wote wanapotekeleza majukumu yao na viongozi wasisite kuchukua hatua stahiki pale watumishi walio chini yao wanapofanya makosa na kutenda kinyume na maadili ya kazi na taaluma zao.

Dkt. Bwana ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana na kusisitiza kuwa viongozi na watumishi wa Umma wanapaswa pia kutambua kuwa wanakazi kubwa ya kuboresha Utumishi wa Umma nchini.

“Bado kuna changamoto kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara na Taasisi za Umma. Kupitia rufaa na malalamiko mbalimbali ya watumishi wa Umma yanayowasilishwa Tume pamoja na Kaguzi zinazofanywa na Tume kuangalia Uzingatiaji wa Sheria katika masuala yanayohusu usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma, Tume imebaini kuwa bado kuna baadhi ya watumishi wa Umma si waadilifu hivyo wanapaswa kujirekebisha na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo na maelekezo halali yanayotolewa na viongozi wao”, alisema.

Akizungumzia ubora katika utoaji wa huduma kwa wananchi, Dkt. Bwana ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazozichukua kuhakikisha kunakuwepo na huduma bora kwa wananchi ili kuwaletea maendeleo Watanzania.

“Wakati haya yanafanyika tuna jukumu kubwa la kuboresha Utumishi wa Umma, wapo baadhi watalalamika kuhusu hatua kali za kisheria zinazochukuliwa. Watailalamikia Serikali na watailalamikia Tume ya Utumishi wa Umma, lakini tunapaswa sote tuungane, watumishi wa Umma na wananchi kwa ujumla. Nchi hii ni yetu sote na maendeleo yataletwa na sisi sote”, alisema.

“Tutambue na kuamua kujenga, kuboresha ama kubomoa. Tutambue hakuna njia ya mkato kufikia maendeleo na kila mmoja wetu kwa nafasi yake anapaswa kuchapa kazi na tusingoje kupata wawekezji wa kuja kutuletea maendeleo. Pale tunapokosea tukubali tumekosea na tujisahihishe”, Alisema.

Aliwataka Waajiri wote nchini kuhakikisha wanatoa mafunzo elekezi kwa watumishi wapya wanapoajiriwa kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu maadili ya kazi, miiko na misingi ya majukumu ya kazi mbalimbali wanazotekeleza. Pia wawasisitizie watumishi kufanya kazi kwa weledi na uzalendo.

 

 

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.