Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Dkt. Mwanjelwa atoa agizo kwa Waajiri

Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu nchini ambao watashindwa kuwasilisha vielelezo vya rufaa zilizokatwa na watumishi wa Umma kwenye Tume ya Utumishi wa Umma ndani ya siku 14 kama sheria inavyoagiza, watachukuliwa hatua kwa kuikwamisha Tume kutekeleza jukumu la kushughulikia kwa wakati rufaa za watumishi.

Tahadhari hiyo imetolewa Dar es Salaam jana na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) alipozungumza na watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma katika ofisi za Tume hiyo.

Dkt. Mwanjelwa alikuwa kwenye ziara ya kikazi yenye lengo la kufahamu kwa kina majukumu ya Tume na kuhimiza uwajibikaji. Alisema kitendo cha Waajiri kutowasilisha vielelezo kwa wakati Tume kunakwamisha jitihada za Tume hiyo kutoa uamuzi kwa wakati kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

Aidha, Dkt. Mwanjelwa ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kuendelea kutoa elimu kwa wadau kwa lengo la kuwawezesha Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika usimamizi wa Rasilimali ili kupunguza malalamiko ya watumishi yasiyo ya lazima.

Naye Mwenyekiti wa Tume Jaji Mstaafu Dkt. Steven Bwana alimshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa maelekezo ya kuboresha utendaji kazi aliyatoa na kuahidi kusimamia utekelezaji wake ili kuhakikisha Utumishi wa Umma unakuwa wenye tija na manufaa kwa Taifa zima.

 

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.