Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Tume ya Utumishi wa Umma yatakiwa kuzingatia weledi, haki na uzalendo katika kushughulikia rufaa za watumishi wa Umma

Serikali imeitaka Tume ya Utumishi wa Umma kuzingatia weledi, haki na uzalendo katika kushughulikia rufaa za watumishi wa Umma zilizofikishwa kwenye Tume hiyo 

Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akifungua mafunzo elekezi ya siku tatu ya Makamishna wapya wa Tume hiyo.

Dkt. Mwanjelwa alisema katika kutoa maamuzi ya malalamiko na rufaa wanapaswa kuzingatia weledi, haki na uzalendo kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma kwa sababu Mhe. Rais ana imani kubwa nao hivyo watekeleze vema majukumu ya Tume ili kuisaidia Serikali ya awamu ya tano kufikia malengo iliyojiwekea ya kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wananchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma Jaji Mstaafu Dkt. Steven Bwana alisema takribani malalamiko na rufaa zaidi ya 100 za watumishi wa Umma zilizofikishwa mbele ya Tume kwa ajili ya kutolewa maamuzi, zitatolewa maamuzi katika kipindi cha muda mfupi ujao. Alisema Tume hiyo anayoiongoza yeye yenye wajumbe saba inaanza rasmi kazi ya kutoa maamuzi ya malalamiko na rufaa hizo kwa kasi na weledi.

Dkt. Bwana alisema uteuzi wao unamaanisha wameaminiwa na Mhe. Rais kufanya kazi hiyo na kwamba hawako tayari kumwangusha kwenye utendaji ndani ya Tume hiyo. “Kazi yetu ni kubwa na ya msingi maana Tume ya Utumishi wa Umma inafanya ukaguzi wa Rasilimali Watu ambayo ni nyezo muhimu katika maendeleo ya Taifa hivyo tunaomba Serikali ituwezeshe vitendea kazi tuchape kazi” alisema.

Tume hiyo mpya inaundwa na Makamishna saba akiwemo Jaji Mstaafu Dkt. Steven Bwana ambaye ndiye Mwenyekiti, Bw. George Yambesi, Alhaji Yahya Mbila. Bibi Immaculate Ngwale, Balozi Mstaafu Daniel Ole Njoolay, Balozi Mstaafu John Haule na Bibi Khadija Mohamed Mbarack. Makamishna hao waliapishwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Januari 09, 2019 Ikulu Jijini Dar es salaam.

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.