Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Watumishi wa Umma waaswa kuzingatia Kanuni za Maadili katika utumishi wao

Watumishi wa Umma wamesisitizwa kuzingatia Kanuni za Maadili katika Utumishi wao ambazo ni pamoja na Kutoa huduma bora, Utii kwa Serikali iliyoko Madarakani, kufanya kazi bila upendeleo, Bidii ya kazi na kufanya kazi kwa uadilifu na weledi pamoja na Matumizi sahihi ya taarifa na nyenzo nyingine za kazi.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Nyakimura Muhoji amesema hayo katika taarifa kwa umma aliyoitoa baada ya Tume ya Utumishi wa Umma kuhitimisha Mkutano wake wa pili kwa mwaka 2017/2018 uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bw. Muhoji amesisitiza kuwa Watumishi wa Umma, Waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu wanapaswa kuzielewa na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayotolewa inayotolewa na Serikali.

“Viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa waelewe, wazingatie na wawaelimishe Watendaji wa Vijiji na Kata kuhusu umuhimu wa uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu wakati wote wanapotekeleza majukumu yao” amesema Bw. Muhoji.

Amebainisha kuwa, katika mkutano huo, Tume ilipokea na kujadili Taarifa za Ukaguzi Maalum wa Rasilimali Watu katika baadhi ya Taasisi za Umma. Taasisi hizo ni; Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Wakala wa Huduma za Ajira (TAESA), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) na Mahakama ya Tanzania.

Akifafanua baadhi ya mambo yaliyobainika kupitia kaguzi hizo na kushughulikia rufaa zilizowasilishwa Tume, Bw. Muhoji amesema kuwa  Tume ilibaini kuwepo kwa ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu miongoni mwa Watumishi wa Umma, Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu. Baadhi ya mambo yaliyobainika ni pamoja na kuwepo kwa tabia na mienendo isiyofaa kwa baadhi ya Watumishi wa Umma ambayo imesababisha watumishi hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Bw. Muhoji ameongeza kuwa mapungufu ambayo Tume imeyabaini katika maeneo mbalimbali ni pamoja na baadhi ya Mamlaka za Nidhamu kushindwa kuwachukulia hatua kwa wakati na kwa mujibu wa Sheria watumishi wenye utendaji usioridhisha walio chini yao; Baadhi ya Mamlaka za Nidhamu kutokuunda Kamati za Uchunguzi au kutotumia Taarifa za Uchunguzi wa awali kama zilivyowasilishwa kwao; Kufungua mashauri ya nidhamu na kukaa muda mrefu pasipo kuyahitimisha; Upungufu katika uandaaji wa Hati ya Mashtaka na uendeshaji wa mchakato mzima wa mashauri. Pia kuajiri na kupandishwa vyeo watumishi bila kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Bwana Muhoji amesema, “Kwa upande wa rufaa Tume  ilijadili na kutoa uamuzi wa rufaa 59, ambapo rufaa 26  zilikataliwa, rufaa 13 zilikubaliwa bila masharti na rufaa 13, zilikubaliwa kwa masharti kuwa mashauri hayo yaanzishwe  upya kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo. Rufaa 5 zilikatwa nje ya muda, hivyo Tume haikuzisikiliza. Rufaa 2 zimeahirishwa kusikilizwa kwa sababu mashauri hayo yanaendelea kusikilizwa Mahakamani.  Aidha, Tume ilipokea na kutolea uamuzi malalamiko 4.  Kati ya hayo malalamiko  3 yalikataliwa na lalamiko 1 lilikubaliwa”.

Kazi kubwa ya Tume ya Utumishi wa Umma ni kusikiliza Rufaa na kurekebu shughuli zote za Rasilimali watu katika Utumishi wa Umma, na kupitia taarifa hiyo Bw. Muhoji ametoa Wito kwa Watumishi wa Umma, Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utekelezaji wa Majukumu yao.

 

Imeandaliwa na:

KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI,

OFISI YA RAIS,

TUME YA UTUMISHI WA UMMA,

05 JANUARI, 2018

 

 

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.