Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Jaji Mst. Mhe. Kalombola ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kugharimia Mradi wa Ujenzi wa Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Mheshimiwa Hamisa Kalombola ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kutoa fedha kugharimia mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma.

Mheshimiwa Kalombola amesema haya hivi karibuni wakati wa ziara ya Makamishna wa Tume kutembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume kuangalia hatua ya ujenzi iliyofikiwa.

“Tumetembelea mradi huu kuangalia hatua iliyofikiwa, tumeridhika na kazi nzuri inayofanyika. Tunampongeza mkandarasi aliyepewa kazi hii kampuni ya CRJE kwa kazi nzuri anayoifanya, tumeona na ametueleza hakuna changamoto yoyote hadi sasa na wanaimani mradi utakamilika kwa wakati. Napenda kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa Serikali kuendelea kutoa fedha za mradi huu ambao unaendelea vizuri na tumemsisitiza mkandarasi CRJE kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati lakini kwa viwango vinavyozingatia thamani ya fedha” amesema Mheshimiwa Kalombola.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, mwakilishi kutoka kwa mtaalam mwelekezi wa mradi huu, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mhandisi Paul amesema hadi tarehe 08 Machi 2024 mradi umefikia asilimia 66 na wanatarajia mradi utakamilika kwa wakati kama ilivyo katika mkataba mwezi Septemba 2024. Aidha, ameshukuru ushirikiano uliopo kati ya Menejimenti ya Tume inayoongozwa na Katibu wa Tume Bw. Mathew Kirama kwa kuhakikisha wakati wote wanakuwa sehemu ya mradi kuangalia hatua iliyofikiwa ya ujenzi, changamoto zinazojitokeza kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja na pia ushiriki katika vikao vinavyofanyika eneo la mradi.

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.