Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Watumishi wa Umma wakumbushwa kuzingatia Sheria

Watumishi wa Umma wamekumbushwa kuzingatia Sheria ili kujiepusha na vitendo vinavyoashiria ukiukwaji wa maadili au uvunjifu wa sheria, hali inayoweza kusababisha Mamlaka zao za Nidhamu kuwachukulia hatua za nidhamu au kuwafikisha mahakamani kwa makosa ya jinai.

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama amesema haya kupitia taarifa kwa vyombo vya habari aliyoitoa baada ya Mkutano wa Tume wa Tatu kwa mwaka wa fedha kuhitimishwa Jijini Dodoma, Mkutano umefanyika kuanzia tarehe 19 Februari 2024 hadi tarehe 08 Machi 2024.

“Tume inatoa rai kwa watumishi wote wa umma, Waajiri, Mamlaka za Ajira na na Mamlaka za Nidhamu kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma ili kujenga taswira nzuri ya Serikali kwa kutoa huduma bora kwa watumishi wenzetu wa umma na wananchi kwa jumla” amesema Bw. Kirama. 

Bw. Kirama akizungumza kuhusu misingi ya haki, amesema ni muhimu kwa Mamlaka za Nidhamu kutambua kuwa moja ya misingi ya kutoa haki ni kwa mtumishi mtuhumiwa kupewa fursa kujitetea kabla ya kuhukumiwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu na Sheria zilizopo. Ni wajibu wa mamlaka hizo kuhakikisha hilo linazingatiwa ili haki si tu itendeke bali ionekane inatendeka kabla, wakati na baada ya usikilizwaji wa mashauri hayo.

“Tume inazikumbusha mamlaka za Nidhamu kuhakikisha kuwa Kamati za Uchunguzi zinazoundwa zinatekeleza wajibu wake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa taarifa zao za uchunguzi zinabainisha iwapo makosa waliyoshtakiwa nayo watumishi watuhumiwa yamethibitika au kutothibitika kutendeka.  Ni muhimu pia kwa Mamlaka za Ajira kujibu barua za maombi ya ruhusa au maombi mengine ya watumishi kwa wakati ili kutowachochea watumishi hao kuvunja sheria au kuwa na malalamiko dhidi yao. Ni wajibu wa mamlaka hizo pia kuhakikisha kuwa stahiki na haki mbalimbali za watumishi zinaheshimiwa ili kupunguza malalamiko ya watumishi waliopo chini yao” amefafanua Bw. Kirama

Bw. Kirama amesema kuwa, Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) ni Idara Inayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais iliyoundwa kwa Mujibu wa Kifungu cha 9 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (Marejeo ya Mwaka 2019). Majukumu ya Tume ni pamoja na kutoa ushauri kuhusu masuala ya usimamizi wa Raslimaliwatu katika Utumishi wa Umma, kushughulikia Rufaa na Malalamiko ya watumishi wa Umma ambao hawajaridhika na uamuzi uliofanywa na Mamlaka zao za Ajira na Nidhamu na kufanya urekebu kwa kuhakikisha kuwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu zinatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Utumishi wa Umma.

“Kwa Mujibu wa Kifungu cha 25 cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 (Marejeo ya Mwaka 2019) kikisomwa kwa pamoja na Kanuni ya 60 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022, Mamlaka za Rufaa katika Utumishi wa Umma zimebainishwa kuwa ni Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Kifungu cha 10(1) (d) na (g) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 (Marejeo ya Mwaka 2019) kimeipa Tume mamlaka ya kupokea na kushughulikia Rufaa na Malalamiko ya Watumishi wa Umma mtawalia ambao hawakuridhika na uamuzi uliotolewa na Mamlaka zao za Nidhamu na Ajira” imeeleza taarifa hiyo.

Katika Mkutano wa Tatu wa Tume, jumla ya Rufaa na Malalamiko 342 yaliwasilishwa na kutolewa uamuzi ambapo Rufaa 160 zilisikilizwa na kutolewa uamuzi na Malalamiko 182 yalisikilizwa na kutolewa uamuzi.  Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya 62(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, Warufani 21 na Mrufaniwa mmoja (01) walitumia haki yao ya kisheria kufika  mbele ya Tume na kutoa ufafanuzi wa hoja zao za rufaa na malalamiko.

Katika Mkutano huo wa Tatu wa Mwaka 2023/2024, makosa yaliyoonekana kutendwa zaidi ni pamoja na; utoro kazini, kuajiriwa bila kuwa na sifa, kukiuka Maadili ya Utumishi wa Umma, wizi, uzembe na kushindwa kutekeleza majukumu na kusababisha hasara kwa Mwajiri.

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.