Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

MRADI WA UJENZI WA JENGO LA OFISI YA TUME YA UTUMISHI WA UMMA UTAKAMILIKA KWA WAKATI

Mhandisi Kelvin Chuma kutoka  Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) amesema ana imani mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma unaoendelea katika mji wa Serikali Mtumba, Dodoma utakamilika kwa wakati.

Mhandisi Chuma amesema haya leo Alhamis tarehe 25 Januari 2024 wakati akiongoza Kikao cha “Site meeting” kilichofanyika eneo la mradi mji wa Serikali, Mtumba ambapo pamoja na mambo mengine mkandarasi CRJE (EA) LTD aliwasilisha taarifa ya utekelezaji na hatua iliyofikiwa katika mradi huu.

“Mwenendo wa utekelezaji wa mradi huu ni mzuri, ninaamini kwa mujibu wa mpango kazi, mradi wa jengo hili la Tume utakamilika kwa wakati kama hakutatokea majanga yoyote. Ninamshukuru “client” anatoa ushirikiano mkubwa kila tunapomhitaji na anajitoa kuhakikisha mradi unaenda vizuri. Kwa upande wa mkandarasi, CRJE hadi sasa anafanya vizuri, hatua kwa hatua na naamini ataendelea kufanya kazi kwa kuzingatia ubora na muda wa mradi.” amesema Mhandisi Chuma.

Kwa upande wake, mhandisi Winkie Paul kutoka CRJE (EA) Ltd amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi namba 13 kuwa hadi sasa mradi umefikia asilimia 65 na kazi zinaendelea kufanyika kadri ya mpango kazi uliopo katika mkataba wa mradi.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu katibu wa Tume, Bw. John Mbisso amesema baada ya kutembelea mradi ameona kazi nzuri inayoendelea kufanyika na amesisitiza masuala ya msingi yaliyojadiliwa na kukubaliana kwa pamoja wakati wa kikao yafanyiwe kazi na mwisho wa siku lengo lililokusudiwa liweze kufikiwa.

Mradi wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Tume ya Utumishi wa Umma ulikabidhiwa kwa mkandarasi  CRJE (EA) Ltd tarehe 15 Desemba 2022, kipindi cha mradi ni miezi 20, ulianza kutekelezwa tarehe 12 Januari 2023 hadi sasa muda wa utekelezaji wa mradi ni miezi 12 na umepangwa kukamilika baada ya miezi nane ijayo ifikapo tarehe 11 Septemba 2024.

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.