Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

WATUMISHI WA MAMLAKA ZA SERIKALI ZA MITAA WAKUMBUSHWA KUHUSU UZINGATIAJI WA MAADILI KATIKA UTENDAJI WAO WA KAZI

  

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Mhe. Hamisa Kalombola amesema watumishi wa umma wanapaswa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maadili wakati wa kutekeleza majukumu yao. 

Mheshimiwa Kalombola amesema hayo Jijini Mwanza wakati akifunga mafunzo ya Kanda ya Ziwa yaliyoandaliwa na Tume ya Utumishi wa Umma kwa washiriki kutoka  Mamlaka za Serikali za Mitaa.

“Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati akiwaapisha Makamishna wa Tume, Ikulu Chamwino Dodoma aliielekeza Tume ya Utumishi wa Umma kuhakikisha watumishi wa umma wanakumbushwa kuhusu uzingatiaji wa maadili katika utendaji kazi wao wa kila siku. Ili kuhakikisha maagizo ya Mhe. Rais yanatekelezwa, Tume imejiwekea mkakati wa kuelimisha na kutoa mafunzo kwa wadau wake ambao ni watumishi wa umma kukumbushana umuhimu wa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na Maadili wakati wa kutekeleza majukumu yao”. Alisema Mheshimiwa Kalombola.

Mheshimiwa Kalombola alisema Tume ina imani kuwa kupitia Kikao Kazi hiki imefanikiwa kuwakumbusha washiriki kuhusu uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika usimamizi wa masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma.

Akifunga kikao kazi hiki,  Mheshimiwa Kalombola amesema Tume inawakumbusha na kuwasisitiza Watumishi wa Umma kuzingatia masuala yafuatayo;- Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuacha kufanya kazi kwa mazoea na wahakikishe wanachukua hatua za kinidhamu kwa Watumishi wa Umma wanaokiuka maadili ya Utumishi wa Umma; Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuhakikisha wanajibu barua au kutoa ufumbuzi na ufafanuzi kwa masuala ya kiutumishi kwa watumishi walio chini yao kwa wakati na  Watumishi wa Umma wanapaswa kusoma na kuzielewa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali  iliyopo. Serikali kupitia Waziri mwenye dhamana na Utumishi alisaini Marekebisho ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, nasisitiza kusoma na kuelewa vizuri Kanuni ya 61(4) inayohusu Tume kuanza kutoa uamuzi kwa kutumia vielelezo vya upande mmoja.

 

Kikao kazi hiki kimefanyika kati ya Tume ya Utumishi wa Umma na washiriki kutoka  Mamlaka za Serikali za Mitaa, waliopo katika Kanda ya Ziwa na kimefanyika katika ukumbi wa Rocky City Mall, Jijini Mwanza.

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.