Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ofisi ya Rais
Tume ya Utumishi wa Umma
Tume ya Utumishi wa Umma ni miongoni mwa Taasisi za Umma ambazo
zimekabidhiwa hati za vibali vya ujenzi wa Ofisi za Taasisi Dodoma.
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew M. Kirama amekabidhiwa
hati hiyo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na
Uratibu) Mhe. George B. Simbachawene (Mb) katika hafla iliyofanyika
Ukumbi wa Hazina Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Waziri Simbachawene (Mb) amesema
lengo la hafla hii fupi ya kukabidhi vibali vya ujenzi kwa Taasisi
zilizopewa idhini ya ujenzi wa Ofisi Dodoma kama sehemu ya kutambua
mchango wa Taasisi hizo katika kuunga mkono utekelezaji wa Mpango wa
Serikali kuhamishia shughuli zake Jijini Dodoma hasa kwa kuzingatia kuwa
Ofisi ya Waziri Mkuu ndio yenye wajibu wa uidhinishaji wa vibali vya
ujenzi wa Taasisi za Serikali katika Makao Makuu ya Nchi.
Mheshimiwa Simbachawene amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea
kutekeleza kikamilifu Mpango wa kuhamia Dodoma ambapo Wananchi wanapata
huduma zote katika Makao Makuu ya Nchi. Aidha, watumishi wote wa
Serikali ikiwemo Wizara zote, Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Mhimili wa
Bunge na baadhi ya Taasisi wamehamia Dodoma na wanaendelea kutekeleza
majukumu yao.
Akizungumzia Sheria ya kuitambua Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi
(Capital City Declaration Act of 2018) alisema ilipitishwa na Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu Septemba 2018 na majengo yote ya
Wizara na Taasisi za Serikali yanaendelea kujengwa Dodoma badala ya Dar
es Salaam.
Majengo haya ya Taasisi yanajengwa katika maeneo ya NCC link, Medeli,
Njedengwa, Mtumba na Kikombo na yanajengwa kwa kufuata Mwongozo uliopo
katika Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma ambao Ofisi ya Waziri Mkuu ina
jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wake.
Mheshimiwa Simbachawene ametoa taarifa kuwa pamoja na ujenzi wa Ofisi za
Taasisi unaoendelea, Serikali imekamilisha ratiba na Mwongozo
utakaowezesha Taasisi za Serikali ambazo bado zinaendelea kutekeleza
majukumu yake Dar es Salaam kuweza kuhamishia shughuli zao Jijini Dodoma
kwa awamu.
"Katika utekelezaji wa suala hili, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa
maelekezo kwamba Taasisi 42 zihamie Dodoma ndani ya mwaka huu wa fedha
2022/2023. Taasisi 36 zitahamia Dodoma katika mwaka ujao wa fedha wa
2023/2024 na Taasisi 19 zitahamia katika mwaka wa fedha 2024/2025 wakati
Taasisi 27 zimeelekezwa kwamba kwa kuzingatia aina ya majukumu
zilizonazo, kuendelea kutekeleza majukumu yao Mkoani dar es Salaam.
Hatua hii itakamilisha sehemu kubwa ya Mpango wa Serikali wa kuhamia
Dodoma ambapo hadi sasa tayari Taasisi 65 zilishahamia Dodoma tangu
mwaka 2016 hadi 2022".
Mheshimiwa Simbachawene ametoa wito kwa Viongozi wa Mkoa wa dodoma,
Wizara, Halmashauri, Taasisi za Serikali, Sekta Binafsi, Wananchi na
wadau wengine kuendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa Mpango
wa Serikali wa kuhamia Dodoma.
Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.