Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

UTEKELEZAJI WA KANUNI YA 61(4) YA KANUNI ZA UTUMISHI WA UMMA ZA MWAKA 2022 KUTATUA CHANGAMOTO YA WATUMISHI WA UMMA

  

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) Mheshimiwa Abdallah Chaurembo Kanuni ya 61(4) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022 itawezesha kutatua changamoto ya watumishi wa umma, kwani kanuni hiyo imetungwa kuiwezesha Tume ya Utumishi wa Umma kutoa uamuzi wa mashauri ya kinidhamu kwa kutumia vielelezo vya upande mmoja ikiwa upande mwingine utachelewesha vielelezo bila sababu za msingi.

Mhe. Chaurembo ametoa maelekezo hayo hivi karibuni Jijijni Dodoma, wakati akiongoza kikao kazi cha kamati yake kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa mwaka 2021/2022.

Mhe. Chaurembo amesema, ni wajibu wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI kuhakikisha Kanuni hiyo inatekelezwa kama ilivyokusudiwa ili iwe na tija, ikizingatiwa kwamba wapo baadhi ya Waajiri, Viongozi na watu wenye Mamlaka wanaokiuka kwa makusudi taratibu za kuwaachisha kazi watumishi wa umma na kuamua kutowasilisha vielelezo vya mashauri ya kinidhamu Tume ya Utumishi wa Umma ili vitumike kutolea maamuzi.

“Ni wazi kuwa Kanuni hii ya 61(4) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2022 inaenda kutatua tatizo la watumishi wa umma kuonewa na kwa kufanya hivyo, mtakuwa mmeunga mkono kwa vitendo dhamira njema ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watumishi wote wanatendewa haki na hatimaye kufanya kazi kwa amani na morali ya hali ya juu katika kuwahudumia wananchi,” Mhe. Chaurembo amesisitiza.

Akizungumzia changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma, Mjumbe wa Kamati ya USEMI ambaye pia ni Mbunge wa Urambo, Mhe. Margaret Sitta amehoji uwepo wa Idara au Kitengo maalum katika Ofisi ya Rais-UTUMISHI ambacho kimepewa jukumu la kushughulikia malalamiko ya Watumishi wa Umma kwa wakati kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akielekeza mara kwa mara.

Akijibu hoja iliyowasilishwa na Mhe. Sitta, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema Ofisi yake ina Idara ambazo zinasimamia ushughulikiaji wa malalamiko katika Utumishi wa Umma ambazo ni Idara ya Usimamizi wa Maadili, Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma na Kitengo cha Sheria pamoja na Tume ya Utumishi wa Umma ambayo inashughulikia rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma.

Aidha Mhe. Ndejembi ameongeza kuwa ofisi imeanzisha Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Centre) kwa ajili ya kuwawezesha watumishi wa umma na wananchi kuwasilisha malalamiko yao pamoja na Mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI ambao unatoa fursa kwa watumishi wa umma na wananchi kuwasilisha malalamiko yao ili yaweze kufanyiwa kazi.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) imepokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya kamati hiyo katika kusimamia utendaji kazi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 

Taarifa Kwa Vyombo vya Habari

31-05-2022

TAARIFA KWA UMMA

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.