Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

MIONGOZO INAYOANDALIWA NA TUME ITAWASAIDIA WAAJIRI, MAMLAKA ZA AJIRA NA MAMLAKA ZA NIDHAMU KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA UFANISI

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma Bw. Mathew Kirama amesema kuwa Miongozo inayoandaliwa na Tume itawasaidia Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa na Serikali.
Bw. Kirama amesema hayo Mkoani Morogoro wakati akifungua kikao kazi cha Tume na wadau wake kinachofanyika ili kupitia na kuandaa Miongozo mbalimbali inayotolewa na Tume.
“Kikao kazi hiki kinafanyika ili kutekeleza moja ya majukumu ya Kisheria ya Tume kama yalivyoainishwa chini ya Kifungu cha 10 (1) (C) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298; Jukumu hili ni la kutoa Miongozo na kufuatilia uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika Utumishi wa Umma. Wote tunafahamu kuwa kwa nyakati tofauti kuna mabadiliko mbalimbali ya Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma yamefanyika, hali ambayo imesababisha Miongozo iliyoandaliwa na kutolewa na  Tume kuwa ni ya kipindi kirefu  na haiendani  na mahitaji halisi ya wakati huu” alisema Bw. Kirama.
Akizungumzia umuhimu wa Miongozo hii, Bw. Kirama amesema kuwa itawasaidia Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa na Serikali litatimia.
Bw. Kirama amefafanua kuwa kikao kazi hiki kinafanyika ili kupitia na kujadili Miongozo ya Tume iliyohuishwa ambayo ni Mwongozo wa Ajira katika Utumishi wa Umma, Mwongozo wa Nidhamu, Rufaa na Malalamiko na Mwongozo wa Kuwasilisha Taarifa Tume ili kuweza kupata maoni na mtazamo wa Wadau kuhusu masuala ya msingi yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kukamilisha kazi ya kuandaa Miongozo husika.  
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti wa Tume, Bw. Evarist Mashiba amesema kuwa kwa kipindi kirefu, Mamlaka mbalimbali zimekuwa na changamoto katika kutekeleza majukumu yake kwa kuwa Miongozo iliyopo imepitwa na wakati kufuatia mabadiliko mbalimbali ya Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, Tume inaona ni muda muafaka kuhuisha Miongozo yake.
Wadau wanaoshiriki katika Kikao kazi hiki ni Ofisi ya Rais Ikulu; Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora;  Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI); Mahakama Kuu ya Tanzania; Ofisi ya Msajili wa Hazina; Tume ya Utumishi wa Walimu; Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma; Taasisi ya Utafiti  wa Misitu Tanzania (TAFORI); Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro;  Halmashauri  ya Manispaa ya Morogoro;  Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma. 

Taarifa Kwa Vyombo vya Habari

31-05-2022

TAARIFA KWA UMMA

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.