Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

"SIMAMIENI HAKI WAKATI WA KUTOA UAMUZI WA MASHAURI YA NIDHAMU" MHE: WAZIRI JENISTA MHAGAMA (MB).

  

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kusimamia haki wakati wa kutoa maamuzi ya mashauri ya nidhamu ya watumishi wa umma yanayowasilishwambele yake  ili kutolewa uamuzi. 

Mhe. Jenista ametoa nasaha hizo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, kilichofanyika ofisini kwake kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika Tume ya Utumishi wa Umma.

Mhe. Jenista ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kutoa maamuzi ya mashauri yote ya kinidhamu kwa kuzingatia haki, kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma iliyopo.

Waziri Jenista ameongeza kuwa, Tume isipo yashughulikia mashauri ya kinidhamu kwa haki na kwa wakati, inakwamisha maendeleo ya nchi yasipatikane kwa wakati na ndio maana Serikali imekuwa ikiihimiza Tume ya Utumishi wa Umma kutekeleza wajibu wake kutolea uamuzi mashauri yaliyo mbele yake kwa kwa haki na kwa wakati.

 “Jambo la msingi hakikisheni haki inatendeka katika mashauri ya kinidhamu, mkifanya hivyo mtakuwa mnasimamia na kujenga nidhamu nzuri ya utendaji kazi katika Utumishi wa Umma,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Aidha, Mhe. Jenista amezungumzia changamoto ukiukwaji wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo  ya utumishi wa umma unaofanywa na baadhi ya waajiri na watumishi, hivyo amewataka Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma kufanyia kazi changamoto hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma, Mhe.  Balozi John Haule amemshukuru Mhe. Jenista Mhagama kwa kuwahimiza kutenda haki wakati wa kushughulikia mashauri ya kinidhamu na kumuahidi kuwa watatoa maamuzi ya mashauri ya kinidhamu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo katika Utumishi wa Umma.

Tume ya Utumishi wa Umma imeundwa chini ya kifungu Na. 9 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298. Tume hii ina jukumu la kufuatilia na kusimamia uendeshaji wa shughuli za rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Utumishi wa umma unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu.

Taarifa Kwa Vyombo vya Habari

31-05-2022

TAARIFA KWA UMMA

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.