Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

WATUMISHI WA TUME YA UTUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUISHI KWA MUJIBU WA VIAPO VYAO KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma,Jaji Mstaafu Mheshimiwa Hamisa Hamis Kalombola amewataka watumishi wa Tume hiyo kuhakikisha wakati wote wanaishi na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Viapo vyao walivyoapa na wakati wote wahakikishe wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Uzalendo, Maslahi ya Taifa, Maadili, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayosimamia Utumishi wa Umma.

Mheshimiwa Jaji Mstaafu Hamisa Hamis Kalombola amesema haya jana Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha baadhi ya Viongozi wa Menejimenti ya Tume walioteuliwa au kuhamia Tume kushika nafasi mbalimbali za Uongozi na Watumishi waliohamia Tume ambao kwanza wanatakiwa kuapa ili waweze kutekeleza majukumu mbalimbali ya Tume.

“Msiishie kuapa tu, mmefika hapa na kusimama mbele yangu kula kiapo cha utii na uaminifu kwa Mamlaka na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa mtatekeleza majukumu yenu ipasavyo. Tambueni kuwa viapo vyenu hivi vina maana kubwa na ni vizito, si kuwa mnaapa tu hapana, miongoni mwenu mmeshika Vitabu vya Dini zenu na mmeapa na kuthibitisha. Niwaombe sana mkafanye kazi kwa uaminifu mkubwa na kwa maslahi ya Taifa, jiepusheni na vitendo vya rushwa na mkaongozwe na uzalendo kwa nchi yenu. Hakikisheni wakati wote mnaishi katika viapo vyenu kwa kuzingatia maadili na kuepuka vitendo vyote visivyofaa, nendeni mkafanye kazi” alisema Mheshimiwa Jaji Mstaafu Kalombola.

Kwa upande wake, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M. Kirama alisema Watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma wanaapishwa katika kipindi hiki ambacho Mwenyekiti na Makamishna wa Tume pamoja na Sekretarieti ya Tume wanashiriki katika Mkutano wa Tume namba 2 kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 unaoendelea kufanyika Jijini Dodoma.

“Uapisho huu kwa Watumishi wa Tume unafanyika kwa mujibu wa  Kifungu cha 11 (3) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 [Marejeo ya mwaka 2019] kinachofafanua kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma akiona inafaa anayo Mamlaka ya kumuapisha au kumthibitisha Afisa yeyote wakati wa kutekeleza majukumu ya Tume” alisema Bw. Kirama.

Mkutano huu wa Tume namba 02 kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 unaendelea kufanyika Jiji Dodoma, na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 08 Julai 2022 ambapo Rufaa na Malalamiko mbalimbali ya watumishi wa umma yaliwasilishwa Tume wakipinga uamuzi uliotolewa na Mamlaka  zao za Ajira na Nidhamu katika Utumishi wa Umma.

 

Taarifa Kwa Vyombo vya Habari

31-05-2022

TAARIFA KWA UMMA

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.