Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

TUME INA JUKUMU LA KUHAKIKISHA WAAJIRI, MAMLAKA ZA AJIRA, MAMLAKA ZA NIDHAMU NA WATUMISHI WA UMMA WANATEKELEZA MAJUKUMU KWA KUZINGATIA SHERIA

Bibi Celine M. Maongezi, Kaimu Naibu Katibu, Idara ya Uzingatiaji na Ukaguzi wa Rasilimali Watu, Tume ya Utumishi wa Umma amesema katika jukumu  la urekebu linalotekelezwa na  Tume, Tume ina wajibu wa kuhakikisha kuwa Waajiri, Mamlaka ya Ajira na Mamlaka ya Nidhamu pamoja na Watumishi wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa ya usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma. Bibi Maongezi amesema haya hivi karibuni katika kituo cha redio cha 92.9 A Fm, Dodoma.

Kaimu Naibu Katibu, Bibi Maongezi amesema kuwa Serikali ilitoa Waraka wa Utekelezaji wa Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002, ambapo ulifafanua kuwa Tume hii itakuwa Tume Rekebu na sio Tendaji.  Hii ina maana kuwa itaendelea na majukumu yake yaliyoko katika Kifungu Na. 10 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298.

Alisema kuwa Tume hufanya Ukaguzi wa masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kubaini kiwango cha uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu katika usimamizi wa Rasilimali Watu kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu. Alifafanua kuwa Ukaguzi huu unaweza kuwa ni wa Kawaida au Maalum.

Alisema kuwa Ukaguzi wa Kawaida, hufanyika kila baada ya mwaka wa fedha kuisha. Ukaguzi huu umelenga kuangalia masuala ya kiutumishi yaliyotengewa fedha katika mwaka wa fedha husika kama yametekelezwa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu na watumishi wamepata stahili zao.

Akifafanua kuhusu  Ukaguzi Maalum, alisema Ukaguzi  huu hufanyika kufuatia Maagizo ya Mkuu wa Utumishi wa Umma au kuombwa na Mamlaka nyingine kufanya hivyo hasa pale ambapo wanapata malalamiko ya Watumishi wa Umma.  Lengo la ukaguzi maalumu ni kubaini ukweli wa malalamiko yaliyowasilishwa, kurekebisha upungufu uliopo kabla ya athari zaidi.


Kwa upande wake, Bw. Robert Lwanji, Afisa Mwandamizi kutoka Kitengo cha Miongozo, Uwezeshaji na Utafiti , Tume ya Utumishi wa Umma alisema Ukaguzi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma una umuhimu mkubwa kwa Serikali kwa sababu huisaidia Serikali na Tume kubaini mambo yafuatayo:-

i)  Iwapo uamuzi uliofanywa na Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kama umefuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa.
ii)  Kiwango cha uzingatiaji katika usimamizi  na  uzingatiaji wa masuala ya Rasilimali Watu.
iii)  Haki imetendeka katika kufikia uamuzi (mwajiri na mtumishi).
iv)  Kuisaidia Tume kutoa mapendekezo ya kuboresha (Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu).

Bw. Lwanji alitumia fursa hiyo kuwakumbusha Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu kuwa wana wajibu wa kuhakikisha  wakati wote wanashughulikia masuala ya Kiutumishi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo  ili kuboresha utendaji wao na hatimaye kutoa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wa Watumishi wa Umma alisema, wana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uaminifu, uadilifu, utii kwa Serikali iliyoko madarakani kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma. 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.