Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Maswali yaulizwayo Mara kwa Mara

Tume ni Mamlaka ya Rufaa kwa Watumishi wa Umma, ni misingi ipi Tume inatumia katika kuamua Rufaa inayowasilishwa mbele yake?

Kwa mujibu wa Kifungu cha 23 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (Marejeo ya mwaka 2019) kimeainisha mambo matatu muhimu ya kuzingatia wakati wa kushughulikia mashauri ya nidhamu kwa watumishi wa umma. Misingi hiyo ni:- i) Mtumishi mtuhumiwa kupewa Hati ya Mashtaka na Notisi. ii) Mtumishi mtuhumiwa kupewa fursa ya kusikilizwa na Kujitetea. iii) Kuundwa kwa Kamati ya Uchunguzi wa shauri endapo mtumishi mtuhumiwa atakana kosa.

2. Tume kama chombo cha kutoa Haki, mtumishi wa umma anategemea kupata nini anapoleta suala lake Tume ya Utumishi wa Umma?

Mtumishi wa Umma anapowasilisha Rufaa yake Tume, atarajie mambo mawili ambayo ni kukubaliwa au kukataliwa kwa rufaa yake. i) Rufaa kukubaliwa Kuna aina mbili za kukubaliwa kwa rufaa ya mtumishi wa umma. Ambayo ni:- ● Kukubaliwa bila masharti ni pale ambapo tuhuma dhidi ya mrufani hazijathibitika na mchakato wa masuala ya nidhamu ulifuata taratibu zote. Kwa hiyo, uamuzi wa Tume unakuwa, Rufaa ya Mtumishi wa Umma imekubaliwa arejeshwe kazini na kulipwa haki zake zote, au apewe tuzo kulingana na adhabu aliyopewa. ● Kukubaliwa kwa masharti ni pale ambapo tuhuma dhidi ya mrufani hazikuthibitika ama mchakato wa masuala ya nidhamu haukuzingatia haki za msingi za mtumishi mtuhumiwa. Kwa hiyo, uamuzi wa Tume unakuwa Rufaa imekubaliwa na Tume inaiagiza Mamlaka ya Nidhamu shauri lianze upya kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu. Kwa mujibu wa Kanuni ya 62 (3) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009. ii) Rufaa kukataliwa Rufaa ikikataliwa ni pale ambapo tuhuma zimethibitika na mchakato wa masuala ya nidhamu ulifuata taratibu zote. Uamuzi wa Tume ni kwamba Rufaa imekataliwa na Tume imethibitisha adhabu aliyopewa na Mamlaka ya Nidhamu.

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.