Tume ya Utumishi wa umma ni nini na majukumu yake ni yapi?
Tume ya Utumishi wa Umma ni Idara ya Serikali inayojitegemea iliyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 ( Marekebisho ya mwaka 2019 ). Tume ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake mnamo tarehe 07 January 2004, baada ya Mwenyekiti na Wajumbe (6) kuteuliwa na Mheshimiwa Rais.
Tume hii ni matokeo ya maboresho yaliyotokea Serikaliani, baada ya kutungwa kwa Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002 na kuundwa kwa Tume moja ili kuongeza tija. Tume zilizokuwepo awali zilikuwa ni:- Tume ya Utumishi Serikalini, Tume ya Serikali za Mitaa na Tume na Tume ya Utumishi wa Walimu.
Majukumu ya Msingi
Majukumu yake ya msingi yameainishwa katika kifungu cha 10 (1) cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298 (Marekebisho ya mwaka 2019) kwa ujumla wake katika maeneo makuu matatu:-
- Ushauri
- Kumshauri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora katika kutekeleza majukumu yake aliyopewa kikatiba chini ya Ibara ya 36 kuhusu ujazaji wa nafasi zilizo wazi katika Utumishi wa Umma.
- Kumsaidia Rais katika masuala yote yatakayohusu Utumishi kadri atakavyohitaji
- Urekebu (Regulatory Body)
- Kuhakikisha kuwa Waajiri, Mamlaka za ajira na Mamlaka za Nidhamu wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali iliyopo katika Utumishi wa Umma. Jukumu hili linaelekezwa na Tume kwa :-
- Kutoa Miongozo ya Masuala ya Ajira na Nidhamu ambayo husaidia kuwa na tafsiri sahihi ya utekelezaji wa Sheria katika Utumishi wa Umma.
- Kuwezesha kwa njia ya elimu ya juu ya utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 ( Marejeo ya mwaka 2019 ) kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu na kwa Watumishi wa Umma ili kila mdau ajue haki na wajibu wake katika Utumishi wa Umma.
- Kufanya Ukaguzi wa masuala ya Rasilimali Watu katika Taasisi za Umma kuangalia uendeshaji na usimamizi wa Utumishi wa Umma kama unazingatia Sheria, Kanuni na taratibu zilizopo.
- Kushughulikia Rufaa na Malalamiko
Kupokea na kushughulika Rufaa na Malalamiko ya Watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na Maamuzi yaliyotolewa na Mamlaka zao za Nidhamu.