Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Mkuchika: Maamuzi ya rufaa 138 yalifanyika na malalamiko 504 yalishughulikiwa kupitia mikutano mitatu ya Tume iliyofanyika 2019/20

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Kapt. (Mstaafu) George H. Mkuchika amesema katika kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020 Tume ya Utumishi wa Umma imetekeleza yafuatayo ikiwa ni pamoja na Maamuzi ya rufaa 138 yalifanyika na malalamiko 504 yalishughulikiwa kupitia mikutano mitatu ya Tume iliyofanyika;-

Mheshimiwa Mkuchika, amesema hayo Bungeni, jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2020/21.

Mheshimiwa Mkuchika alisema;-

Mheshimiwa Spika,
Tume ni chombo rekebu na inayo Mamlaka na wajibu wa kuhakikisha kuwa masuala ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma yanasimamiwa na kuendeshwa kwa kuzingatia Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu mbalimbali kama inavyotolewa na Mamlaka. Wajibu huu wa Tume una lengo la kuimarisha Utawala Bora unaozingatia matokeo. Katika kutekeleza wajibu huu pamoja mambo mengine Tume imeendelea kufanya ukaguzi wa  Rasilimaliwatu kwa Mamlaka za Ajira na Nidhamu.

Aidha, Tume ya Utumishi wa Umma ni Mamlaka ya Rufaa kwa Watumishi wa Umma dhidi ya Uamuzi unaotolewa na Mamlaka zao za nidhamu.


Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha Julai 2019 hadi Machi, 2020 Tume imetekeleza majukumu yafuatayo:-

(i) Uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu katika usimamizi wa Utumishi wa Umma umesimamiwa kwa kufanya ukaguzi
katika taasisi 77;

(ii) Maamuzi ya rufaa 138 yalifanyika na malalamiko 504 yalishughulikiwa kupitia mikutano mitatu ya Tume iliyofanyika;

(iii) Elimu kwa wadau kuhusu majukumu ya Tume na Utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma ilitolewa kwa taasisi za umma.
 
Aidha, kupitia ziara ya Makamishna   wa Tume, elimu ilitolewa kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 na haki na wajibu wao kwa watumishi wa umma 1070 wakiwemo Viongozi wa Taasisi za Umma ambao ni Wakuu wa Mikoa (Mwanza na Simiyu), Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya, Watendaji Wakuu wa Wakala za  Serikali, Taasisi za Umma na Watumishi wa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri. Vile vile, elimu ilitolewa kupitia kurusha vipindi sita hewani vya Runinga na vipindi sita vya Redio.

Pia, kupitia maadhimisho ya Siku  ya Maadili na Haki za Binadamu wadau wa Tume walipatiwa elimu  kuhusu Sheria Na. 8 na Kanuni zake;

(iv) Taarifa ya Hali ya Utumishi wa Umma na Utekelezaji wa Majukumu ya Tume ya Mwaka 2018/19 iliandaliwa na kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;

(v) Utekelezaji wa mahitaji ya anuai za jamii katika utumishi wa umma ulifanyika kwa kuwapatia huduma watumishi wa Tume wenye uhitaji
maalum kulingana na Miongozo iliyopo; na

(vi) Watumishi 209 wa Tume wamewezeshwa kupata mafunzo ambapo watumishi 17 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu, watumishi
100 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi katika maeneo ya uadilifu na OPRAS. Vile vile, watumishi 92 walipatiwa mafunzo maalum ya Uchambuzi wa Rufaa na Ukaguzi wa Rasilimali Watu.  

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.