Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Mkuchika: Taasisi zote za Umma zinatakiwa kuwa na Kamati za Kusimamia Uadilifu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa George Mkuchika (Mb) ameziagiza Taasisi zote za Umma kuhakikisha zinakuwa na Kamati za Kusimamia Uadilifu  ili kuweza kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa.
Mheshimiwa Mkuchika ametoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la  kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu tarehe 11 Desemba 2019 lililofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa – Bungeni Dodoma.
“Katika kuimarisha uadilifu katika Sekta ya umma, Serikali pia inatekeleza Mkakati wa Taifa Dhidi ya Rushwa na Mpango Kazi wake ambapo Taasisi zote za Umma zinapaswa kuwa na Kamati za Kusimamia Uadilifu. Mkakati huu ulizinduliwa tarehe 10 Desemba, 2016 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwenye Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu.  Mkakati huu ulianza kutekelezwa rasmi tarehe 01 Julai, 2017. Malengo mahsusi makuu ya Mkakati huu ni:- Kuimarisha ufanisi, uwazi na uwajibikaji wa utoaji wa huduma katika sekta ya umma na sekta binafsi; Kuwa na ufanisi katika utekelezaji wa Mikakati ya Mapambano dhidi ya Rushwa;  Kuzijengea uwezo Taasisi Simamizi za masuala ya Utawala bora; na Kuwa na Uongozi wa Kisiasa madhubuti unaoshiriki kwa dhati katika mapambano dhidi ya rushwa. Ningependa kuchukua fursa hii kuziagiza Taasisi zote za Umma nchini kusimamia utekelezaji wa Mkakati huu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba kila Taasisi inakuwa na Kamati ya Kusimamia Uadilifu ili kuweza kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Mkakati huu.” alisema Mheshimiwa Mkuchika.
Kwa kiasi kikubwa utekelezaji wa Mkakati huu umejikita kwenye Sekta za kimkakati zikiwemo Manunuzi ya umma; Ukusanyaji wa mapato; Utoaji wa haki; Maliasili na utalii; Madini; Nishati; Mafuta na gesi; Afya; Elimu na Ardhi. Mkakati huu unatekelezwa katika ngazi ya Kijiji/Mtaa, Kata, Tarafa, Wilaya, Mkoa na Taifa.
 Mheshimiwa Mkuchika aliwaagiza  Viongozi wote katika Utumishi wa umma kusimamia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya utumishi ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuboresha Utumishi wa Umma ili wananchi waweze kupatiwa huduma bora na bila usumbufu wa aina yoyote. Vilevile, aliwaagiza watumishi wa umma wote kutekeleza majukumu yao  kwa kuzingatia Maadili na Weledi wa Taaluma zao wakiongozwa na Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo na itakayotolewa.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na:-  Mheshimiwa Mary Mwanjelwa (Mb), Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Dkt. Moses Kusiluka - Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu; Mheshimiwa Jaji Mstaafu Harold Nsekela – Kamishna wa Maadili; Bwana Charles Kichele - Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; Mheshimiwa Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu – Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora; Brigedia Jenerali John Mbungo - Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU; Mheshimiwa Balozi Dkt. Marten Lumbanga – Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu; Bwana Nyakimura Muhoji, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma; Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu; Wakuu wa Taasisi za Serikali na Viongozi; Watumishi wa Umma na Waandishi wa Habari.

_________________________
 

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.