Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Watumishi wa Umma kujitathmini siku ya Maadili 2019

Watumishi wa Umma watatumia  Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa kwa kufanya kongamano la kujitathmini kuona wapi wanafanya vizuri na wapi hawafanyi vizuri ili kuboresha ili  lengo la Serikali la kutoa huduma bora kwa wananchi liweze kufikiwa.  Kongamano hili litatoa fursa kwa watumishi wa umma  kujadili kwa kina na mapana masuala yanayohusu Maadili na Haki za binadamu na kuishauri Serikali.
Bibi Celina Maongezi kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Umma amesema hayo katika kipindi leo asubuhi tarehe 09 Disemba 2019 kupitia kituo cha redio  “Nyemo 97.7 fm” jijini Dodoma. Amesema  Kongamano hili litakalofanyika tarehe 11 Disemba, 2019 katika Ukumbi wa Pius Msekwa uliopo Ofisi ya Bunge, Dodoma itakuwa ni fursa kwa washiriki ambao ni watumishi wa umma  kujitathmini na  itasaidia kuona namna ya kuboresha pale ambapo hatufanyi vizuri na kutasaidia pia kuona namna ya kushughulikia kero na malalamiko ya watumishi wa umma.
Akizungumzia Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu amesema  siku hii inatokana na kuunganishwa Siku ya Kimataifa ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa iliyokuwa ikiadhimishwa kila tarehe 9 Desemba, tangu mwaka 2004 kutokana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (United Nations Convention Against Corruption – UNCAC). Mkataba huo ulisainiwa na nchi wanachama wa Umoja huo mjini Merida nchini Mexico tarehe 9 Desemba, 2003. Kwa kuzingatia kwamba Desemba 9 Tanzania huadhimisha Sikukuu ya Uhuru na Jamhuri, mwaka 2005 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kwamba siku hiyo iwe inaadhimishwa tarehe 10 Desemba na Kitaifa iitwe Siku ya Maadili na Haki za Binadamu.

Bibi Maongezi amefafanua kuwa kutokana na Siku hizo kuadhimishwa tarehe moja na kwa kuwa Taasisi zilizokuwa zikiratibu ni za umma, mwaka 2016 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliamua kuunganisha uratibu wa Maadhimisho hayo na uamuzi huo ndiyo uliweka siku inayoitwa “Maadili na Haki za Binadamu”. Iliamuliwa pia kwamba Taasisi zote za umma zinazoshughulika na Maadili, Mapambano dhidi ya rushwa, Haki za binadamu, Uwajibikaji na Utawala bora zishirikiane kuratibu Maadhimisho ya siku hiyo.

Kwa upande wake bwana Mcharo Mrutu kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma “PPRA” amesema, Tanzania imeendelea kufanya vizuri katika masuala ya Haki za Binadamu. Amesema kupitia Haki mbalimbali kama Haki za Kiuchumi, Haki za Jamii, Haki za Kisiasa, Haki za Kiraia kwa kulinganisha na wenzetu nchi jirani, Tanzania tuko vizuri. Huduma mbalimbali ambazo ni Haki za wananchi zimeboreshwa na wanazipata vizuri, mfano kupitia huduma za Afya ambazo ni Haki ya Kijamii ni eneo ambalo pamoja na maeneo mengine kama umeme tunaona kabisa Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha watu wanapata huduma bora. Hata hivyo tunapaswa kufahamu kuwa hakuna Haki bila Wajibu, kila mmoja wetu pale alipo ahakikishe anatimiza wajibu wake vizuri, tusibaki kudai Haki wakati hatutimizi Wajibu wetu.

Kauli mbiu katika Maadhimisho ya mwaka 2019 ni “Maadili katika Utumishi wa Umma ni Nguzo Muhimu katika Kuimarisha Utawala Bora na Haki za Binadamu”. Mgeni Rasmi katika Kongamano hili anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Kapt. (mstaafu) George H. Mkuchika (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.