Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

TUGHE: TUNARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA TUME YA UTUMISHI WA UMMA KATIKA UTOAJI WA HAKI KWA WATUMISHI

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE),  Makao Makuu Taifa, Bwana Shadrack Mkodo, amesema Watumishi wa Umma kupitia Vyama mbalimbali vya Wafanyakazi wanaridhishwa na utendaji wa kazi wa Tume ya Utumishi wa Umma hususan katika kushughulikia rufaa na malalamiko ya Watumishi wa Umma yanayowasilishwa Tume.

Bwana Mkodo amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za TUGHE katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Utumishi wa Umma, kilichofanyika hivi karibuni.

“Vyama vya Wafanyakazi kupitia Mabaraza ya Wafanyakazi, wakati wote tunapokutana katika vikao na mikutano yetu mbalimbali, tunathibitisha kwamba  hakuna malalamiko yoyote ambayo yamekuwa yanatolewa kuhusu utendaji kazi wa Tume ya Utumishi wa Umma, hasa namna inavyoshughulikia na kutoa uamuzi wa rufaa na malalamiko ya watumishi. Tume imekuwa ikitenda haki katika utoaji wa uamuzi wa rufaa na malalamiko yanayowasilishwa mbele yake. Hakuna upendeleo wa aina yoyote wala viashiria vya uwepo wa rushwa” alisema.

Aliwaeleza Wafanyakazi kuwa pamoja na Tume kutenda haki bado kuna umuhimu wa kuongeza mikakati ya utoaji elimu kwa wadau wake mbalimbali, hususan  Wakuu wa Taasisi za Umma na Wakurugenzi.

“Watumishi wa umma wanabadilika mara kwa mara, kuna ambao wanateuliwa na wengine wanaajiriwa. Ni muhimu sana wakapatiwa elimu kuhusu Sheria na Kanuni pamoja na namna ya kuwasilisha rufaa na malalamiko yao Tume, pale wanapohitaji kufanya hivyo” alisema.

Bwana Mkodo alisema Baraza la Wafanyakazi ni hitaji la kisheria ambalo lina lengo la kutoa fursa kwa Watumishi kupitia wawakilishi wao, kujadiliana juu ya masuala mbalimbali ya msingi yanayohusu tija na ufanisi kwa upande mmoja na kwa upande wa pili maslahi ya ustawi wao kama Watumishi wa Umma.

“Mabaraza ya Wafanyakazi sehemu za kazi husaidia kuimarisha ushiriki wa kweli wa Wafanyakazi katika kutekeleza majukumu ya Taasisi. Baraza la Wafanyakazi lina majukumu yake kama yalivyofafanuliwa katika Mkataba wa Kuunda Baraza la Wafanyakazi. Majukumu hayo ni pamoja na kujadili na kushauri Menejimenti  kuhusu Mipango ya Taasisi. Vile vile kujadili na kupitisha Makisio ya Bajeti, Mapato na Matumizi ya Taasisi. Aidha kupitia Baraza la Wafanyakazi, Wajumbe wa Baraza wanayo fursa ya kujadili na kutafakari, si maslahi yao tu, bali pia utendaji wao wa kazi wa kila siku na namna  ya kuuboresha” alisema.

 

 

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.