Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Watumishi wa Umma pelekeni Rufaa na Malalamiko yenu Tume ya Utumishi wa Umma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Kapt. (mstaafu) George H. Mkuchika (Mb) amewataka watumishi wa umma pale wanapoona hawakutendewa haki, wanapokuwa na manung’uniko au malalamiko wanatakiwa kuyapeleka Tume ya Utumishi wa Umma ili kutafuta haki zao.
Mheshimiwa Mkuchika amesema hayo jana wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijni Dodoma ikiwa ni uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 10 Disemba.
“Serikali inapambana kuhakikisha kunakuwa na Utawala bora na ndio maana vyombo vimeundwa na vipo vinafanya kazi zake na Ofisi ya Rais (UTUMISHI) ina jukumu la kuratibu Utawala Bora ndani ya Serikali” alisema.
Akizungumzia Taasisi simamizi zinazoratibu maadhimisho haya alisema Taasisi hizo ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, TAKUKURU, Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali,  Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi  wa Umma na Wizara ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Mkuchika amesema kuwa Watumishi wa Umma wanapaswa kufahamu kuwa kuna mahali wanaweza kwenda kutafuta Haki zao. Tume ya Utumishi wa Umma ni chombo kilichoundwa chenye wajibu wa kuhakikisha kwamba kunakuwepo na Utawala bora katika Usimamizi na Uendeshaji wa masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma ili uweze kutoa matokeo yenye tija na huduma bora inayotarajiwa na Wananchi.
“Watumishi wa Umma wale ambao mnaona hamjaridhika au mnaopinga uamuzi uliotolewa na Mamlaka ya Nidhamu pelekeni Rufaa au Malalamiko yenu Tume ya Utumishi wa Umma, Tume hii  ina wajibu mkubwa wa kuhakikisha  haki inatendeka kwa watumishi wa umma katika Masuala ya Ajira na Masuala ya Nidhamu. Tume hii ilikuwa na Ofisi zake katika jengo la LAPF Ubungo Plaza, kwa sasa wanahamia Ofisi iliyokuwa inatumiwa na Makamu wa Rais, ipo barabara ya Luthuli karibu na Ikulu, jijini Dar es Salaam. Hawa Tume bado wapo Dar es Salaam” alisema Waziri Mkuchika.
Kauli mbiu ya mwaka 2019 katika Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ni “Maadili katika Utumishi wa Umma ni nguzo muhimu katika kuimarisha Utawala Bora na Haki za Binadamu”.

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.