Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais

Tume ya Utumishi wa Umma

Waajiri wasiozingatia Sheria kuadhibiwa - Kamishna

Ofisi ya Rais - Tume ya Utumishi wa Umma imesema haitasita kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu ambao wataendelea kutozingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali inayotolewa na Serikali kusuhu usimamizi wa rasilimali watu katika Utumishi wa Umma.

Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma Bi. Salome Mollel aliyasema hayo jijini Dar es salaam jana ikiwa ni siku chache tangu amalize ziara ya kikazi Mkoani Lindi alikoambatana na baadhi  ya Watendaji wa Tume hiyo.

Katika ziara hiyo alizungumza na Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu katika Sekretarieti ya Mkoa, Halmashauri za Wilaya, Taasisi za Umma na watumishi wa Umma.

Alisema kuna udhaifu mkubwa kwa baadhi ya Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu katika kushughulikia masuala ya kiutumishi ambao unadhoofisha juhudi za Serikali za kuboresha Utumishi wa Umma.

“Hili tumelibaini kupitia ukaguzi wa usimamizi wa uendeshaji wa rasilimali watu katika Utumishi wa Umma tulioufanya katika maeneo mbalimbali nchini na pia uzoefu katika kushughulikia masuala ya rufaa zinazowasilishwa katika Tume ili kutolewa uamuzi”, alisema.

Kamishna huyo pia alibainisha kuwa Utumishi wa Umma una dhamana kubwa ya kuhakikisha huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali kwa wananchi zinatolewa kwa viwango vinavyotakiwa na kwa wakati ili kukuza uchumi wa nchi.

“Endapo hakutakuwa na usimamizi imara wa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo katika usimamizi wa wa rasilimali watu katika Utumishi wa Umma, basi hata huduma zitolewazo kwa wananchi hazitakidhi matarajio ya wengi na uchumi wa nchi utakuwa duni” alifafanua.

Mbali na hilo, alisisitiza ili Utumishi wa Umma ukidhi matarajio ya wananchi ya kupata huduma bora na kwa wakati, Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu wanapaswa kuzisoma, kuzifahamu na kuzisimamia ipasavyo Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ambayo itawasaidia kuamua na kutenda haki kwa usawa.

Hivyo aliwataka Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu katika Mkoa wa Lindi na mikoa mingine watakayozuru, kuzingatia Sheria zinazosimamia masuala ya rasilimali watu ili kuleta maendeleo katika mikoa hiyo.

Kamishna Mollel amewaasa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuchukua hatua kwa wakati dhidi ya maamuzi mbalimbali ya kiutumishi yanayofikiwa dhidi ya watumishi waliokiuka Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

“Sio jambo la busara wala sio uwajibikaji iwapo maamuzi sahihi yanafikiwa halafu hatua za utekelezaji hazichukuliwi kwa wakati” amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa Tume hiyo, Bw. Nyakimura Muhoji aliwataka Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kushughulikia kwa wakati madai mbalimbali ya watumishi ili kuondoa kero na malalamiko ambayo si ya lazima na yanayosababisha Seikali kupakwa matope  pasipo sababu za msingi.

Pia ametoa wito kwa watumishi wa umma kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kuzingatia Mkataba wa Huduma kwa Mteja wa Taasisi husika ili kufikia adhma ya Serikali ya kuboresha Utumishi wa Umma na kufikia uchumi wa viwanda.

Tume ya Utumishi wa Umma ina jukumu la kurekebu Utumishi wa Umma nchini ili kuimarisha utawala bora na uwajibikaji kwa Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu na watumishi. Aidha, Tume hiyo hufuatilia na kutathmini uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma nchini.

 

 

Kurasa za Karibu

Hakimiliki © 2014. Tume ya Utumishi wa Umma. Haki zote zimehifadhiwa.